19 September 2012

SPUTANZA yatishia kuishtaki Simba


Na Andrew Ignas

CHAMA cha Kutetea Haki za Wachezaji nchini (SPUTANZA), kimetishia kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa Klabu ya Simba kutokana na kuwayumbisha wachezaji.


Akizungumza Dar es Salaam jana Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa SPUTANZA, Shaban Geva alisema chama hicho kilipanga kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwapeleka mahakamani viongozi wa Simba kutokana na kitendo cha kutishia kujiondoa katika wa Ligi Kuu Bara.

"Haki ya msingi ya wachezaji ni kucheza kwa kuwa, walisajiliwa kwa ajili ya kucheza hivyo haitawezekana sisi mamlaka husika kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wanaotaka kuwanyima haki hiyo wachezaji," alisema Geva.

Geva ambaye pia ni mwanachama wa Simba, alisema pia analaani vikali usajili wa mabeki, Pascal Ochieng na Kobil Keita kuwa haukuwa na hitaji wakilinganisha na uwezo wa mabeki Juma Nyoso na Shomari Kapombe.

"Licha tu ya kuwa mjumbe wa SPUTANZA, mimi pia ni mwanachama wa Simba mwenye kadi namba 1086, sifikiri kama usajili wa Ochieng na Keita kimsingi una tija kwa kuwa ubora wa Kapombe na Nyoso ni wa juu kuliko wao sasa kwa nini kwa hili nisilipigie kelele,"alihoji.

Wakati huo huo, alisema Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linatakiwa kuhakikisha wachezaji wa kigeni hawapewi kipa umbele kwa kuwa wanachagia kuua soka la ndani.

No comments:

Post a Comment