19 September 2012

Klabu zahimizwa kufika Morogoro



Na Mwali Ibrahim

CHAMA cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA), kimezitaka klabu zitakazoshiriki mashindano ya Klabu Bingwa Taifa, kuhakikisha zinafika mkoani Morogoro Ijumaa kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano Mkuu kabla ya kufanyika michuano hiyo.


Kikao hicho kinatarajia kuwakutanisha makocha, Mameneja wa timu zote kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mashindano hayo, ikiwa ni pamoja na kupanga ratiba.

Mashindano hayo yanatarajia kuanza rasmi Septemba 26, mwaka huu katika Ukumbi wa Bwalo mkoani humo ambapo kutakuwa na timu za Wanaume na Wanawake.

Timu zilizothibitisha kushiriki mashindano hayo kwa wanaume ni mabingwa watetezi Magereza, Jeshi Stars, JKT, Kijichi, Future, Moro Stars, Mzinga, Dodoma, Arusha, Geita na Mbunda.

Kwa wanawake kutakuwa na mabingwa watetezi Magereza, Jeshi Stars, JKT, Kijichi, Moro Stars na Dodoma.

Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo wa TAVA Alfred Selengia, alisema maandalizi yapo katika hatua za mwisho na ratiba itapangwa katika kikao hicho.

"Bingwa katika mashindano haya atashiriki michuano ya Kanda ya Tano ya Afrika Mashariki na Kati, mshindi wa pili mpaka wa nne kwa pande zote watapata nafasi ya kushiriki mshindano ya Muungano mwakanir," alisema.

Alisema mashindano hayo yatafunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi na kufungwa na Mkuu wa Mkoa Joel Bendera.

No comments:

Post a Comment