14 September 2012
Simba 'yakomaa' kumfikisha Yondani polisi
Na Mwali Ibrahim
KAMATI ya Utendaji wa Klabu ya Simba, imedai kuupeleka mkataba wa mchezaji Kelvin Yondan Polisi ili waweze kutambua alama ya kidole gumba aliyoiweka mchezaji huyo kama ni yake au sio.
Kamati hiyo imefikia uaamuzi huo kupitia kikao chake kilichokaa kwa siku mbili mfululizo ikiwa ni pamoja na kujumuisha wanachama wa klabu hiyo baada ya Kamati ya Maadili, Sheria na hadhi ya wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuamua mchezaji huyo pamoja na Mbuyu Twite kuwa ni wachezaji halali wa Yanga.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa habari wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga alisema wameamua kupeleka mkataba huo polisi kutokana na wao kuwa na vifaa vinavyoweza kutambua vidole gumba na wao hawana uwezo huo.
"Siku yoyote suala hili litafikishwa polisi kwa ajili ya kuangaliwa na majibu yatakayopatikana ndio yatatufanya tutoe maamuzi halisi ya klabu hii kwani Yondani alikana kuwa hajasaini mkataba na Simba na kuamua kusaini na Yanga na Kamati ya Sheria ikaidhinisha kuwa mchezaji huyo ni wa Yanga, hivyo wao wanasubiri majibu hayo ndio watoe maamuzi," alisema.
Alisema, pia Simba inaendelea kutafuta haki ya mkataba wa mchezaji huo na ndio maana wamemua kulipeleka suala hilo Polisi kwani nzuri ya kupatikana kwa haki.
Alisema pia katika kikao hicho waliadhimia kuwa hawataweza kujitoa kushiriki katika ligi kuu inayotarajia kuanza hivi karibuni na wapo tayari kushiriki ligi hiyo na mashindano yoyote yatakayoandaliwa na TFF kwani kuamua kujitoa ni sawa na kususa.
Hata hivyo wamekubaliana kuwa wanachama wa Simba waliokuwa na nia ya kuishtaki TFF kupitia kamati yake hiyo kutokana na uamuzi wa kuwaruhusu Yondani na Twite kuchezea Jangwani, suala hilo halitokuwepo tena kwani italeta athari kwa klabu.
Wamewataka wanachama kukaa tayari kwa kupewa taarifa ya kila kitakachoendelea kuhusu suala hilo na wana amini uamuzi waliouchukua ni wa busara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment