14 September 2012

Simba, Azam zaambulia sh. milioni 64.5 Ngao ya Jamii


Na Amina Athumani

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema litatoa vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 7.3 kwa Hospitali ya Temeke mkoani Dar es Salaam ambazo ni asilimia 5 ya fedha zilizopatikana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Azam.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ni kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mwaka  2012/2013.

Alisema mechi hiyo ambayo  ilichezwa Septemba 11 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliingiza sh. milioni 146, 640,000 na kila timu iliambulia sh. 32,265,025.93, .

Alisema jumla ya washabiki 26,001 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Simba kushinda mabao 3-2.

Wambura alisema Sekretarieti ya TFF inatarajia kukutana na uongozi wa Hospitali ya Temeke wakati wowote kuanzia jana ili kujua mahitaji halisi kabla ya kufanya ununuzi wa vifaa husika.

Alisema mgawanyo wa mapato ya mechi hiyo ni asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh.22,368,813.56, asilimia 5 ya mchango wa kusaidia jamii (Hospitali ya Temeke) sh. 7,332,000, uwanja sh. 10,148,318.64, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 4,059,327.46, TFF sh. 10,148,318.46 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,074,159.32.

Alisema Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 1,014,831.86,asilimia 10 ya gharama za mchezo sh. 10,148,318.64, nauli kwa waamuzi na kamishna sh. 80,000  na posho ya kujikimu kwa waamuzi na kamishna sh. 230,000.

Alitaja mgawanyo mwingine ni posho ya waamuzi sh. 400,000, tiketi sh. 4,495,800, maandalizi ya uwanja sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi uwanjani sh. 2.350,000 na Wachina ni sh. 2,000.000.

Wambura alisema mchango wa kusaidia jamii kwenye mechi ya Ngao ya Jamii kuzindua msimu uliopita kati ya Yanga na Simba ulikuwa sh. milioni 15,000,000 ambazo zilikwenda Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) kusaidia uchunguzi wa kansa ya matiti kwa akina mama.

No comments:

Post a Comment