24 September 2012

Simba we acha tu



Na Speciroza Joseph

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, timu ya Simba, imeendeleza wimbi lake la ushindi baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Simba imerudi kileleni mwa ligi hiyo kwa kufikisha pointi tisa mbele ya Azam FC yenye pointi saba ikifuatiwa na Coastal Union ya Tanga yenye pointi tano sawa na JKT Oljoro ya Arusha ila zinatofautiana kwa mabao.

Katika mechi hiyo, Simba ilianza kuliandama lango la Ruvu kwa shambulizi la kushtukiza dakika ya nane, na kupata faulo iliyopigwa na Mrisho Ngassa lakini mpira ulitoka sentimeta chache langoni mwa Ruvu.

Dakika tatu baadaye, Daniel Akuffor wa Simba alipiga shuti nje ya eneo la hatari na kuokolewa na kipa Benjamin Haule na kuwa kona tasa huku Ruvu nayo ilijibu shambulizi hilo dakika ya 23 kupitia kwa Said Dilunga akiwa ndani ya eneo la hatari lakini alishindwa kufunga baada ya kupiga shuti dhaifu.

Mshambuliaji Felix Sunzu ambaye alizikosa mechi mbili za kwanza, aliifungia Simba bao la kuongoza kwa kichwa dakika ya 29 akiunganisha krosi iliyopigwa na Said Nassor 'Cholo' na kumuacha kipa Haule akiruka bila matarajio.

Ikiwa imebaki dakika chache kabla ya mapumziko, Akuffor aliikosesha Simba bao la pili baada ya mkwaju wake wa penalti aliopiga kupanguliwa na Haule, kutokana na beki wa Ruvu kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Ruvu ikionekana kutaka kusawazisha ambapo ilifanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa Simba na dakika ya 76, Seif Rashid aliyeingia badala ya Paul Ndauka aliisawazishia timu hiyo kwa kumtoka Juma Nyosso na kukwamisha mpira wavuni.

Baada ya kufungwa bao hilo, Simba ilitulia na kufanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa Ruvu ambapo dakika tano kabla ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, Edward Christopher aliyeingia badala ya Akuffor aliifungia Simba bao la pili akimalizia krosi ya Ngassa.

No comments:

Post a Comment