13 September 2012
Mwamko mdogo utawala bora unazorotesha maendeleo
Na Rehema Mohamed
UTAWALA bora ni mfumo unaotakiwa kufuatwa na jamii ili kuweza kuwa na maendeleo endelevu yenye uwazi, ukweli na
uwajibikaji.
Lengo kuu la utawala bora ni kupunguza umaskini kupitia uongozi bora, uongozi bora, mipango na utekelezaji wake ambao husimamia rasilimali za Taifa.
Ili kujiletea maendeleo, dhana nzima ya utawala bora
inatakiwa kuanzia ngazi ya chini ya uongozi hadi juu
ili nchi iweze kufikia malengo iliyojiwekea.
Kutokana na umuhimu huo, shirika lisilo la kiserikali
la Pamoja Daima (PADA) kwa kushirikiana na shirika
la Civil Society foundation limeanzisha mradi wa
utawala bora kwa viongozi wa serikali za vijiji
katika Wilaya ya Kisarawe.
Kupitia uongozi wa kijiji kuanzia Mwenyekiti wa kijiji, Afisa Mtendaji wa kijiji, Halmashauri ya kijiji yenye wajumbe 15 au wasiozidi 25, Kamati ya uchumi, mipango na fedha, Kamati ya huduma ya jamii na shughuli za kujitegemea, kamati ya ulinzi na usalama pamoja na wananchi kuwajengea uwezo wa utawala bora.
Miongoni mwa vijiji hivyo ni vile vya Kata ya Malumbo Wilayani humo ili kuhakikisha kuwa dhana ya utawala bora inatekelezeka.
Kata hiyo inajumuisha kijiji cha Palaka, Kitonga,
Marumbo na Kidugaro cha Kanga.
Maratibu wa Mradi huo kutoka PADA Bw.Hamza Sung'he anasema mradi huo unaendeshwa kwa kutoa semina elekezi kwa viongozi mbalimbali wa vijiji, watendaji, wajumbe wa kamati ndogondogo za maendeleo na za uadilifu .
Bw.Sung'he anasema kuwa lengo la mradi huo ni kuongeza uewelewa kwa viongozi wa serikali za vijiji, wananchi na wajumbe wa kamati ndogondogo za utawala bora katika jamii.
Bw.Sung'he anasema, wanafundishwa jinsi ya kuboresha mahusiano kati ya viongozi, wananchi na serikali za vijiji husika.
Anasema, viongozi wa vijiji husika wanajua majukumu yao na kuwajibika kuleta maendeleo kwa wananchi wao.
Mkufunzi wa viongozi wa vijiji katika mradi huo Bw.Abraham Silumbi anasema walichokigundua katika Wilaya hiyo ni kwamba elimu zaidi ya uraia inahitajika katika kipindi cha uchaguzi wa viongozi wa vijiji kwakuwa viongozi wengi hawana uewelewa wa kutosha.
Anasema kuwa hiyo ni kutokana na kubaini kwamba wananchi wengi huchagua viongozi wao wa vijiji kwa umaarufu, kujuana na hawapimi kiongozi anayewafaa na kuwasaidia katika kuendesha masuala yao ya kuwaletea maendeleo.
"Tumeona wakati tunapitia mada mbalimbali za uongozi na majukumu ya kamati za kijiji katika serikali hizo na mitaa, tumeoana baadhi ya kamati zimeundwa kwa uzoefu tofauti na maelekezo ya muongozi wa utawala bora zinavyoelekeza," anasema Bw.Silumbi.
Bw.Silumbi anasema kutokana na kasoro hiyo, viongozi
waliochaguliwa hawajitumi, na wamekuwa wakikaa huku
wakisubiri kuletewa kila kitu.
Anasema viongozi wenye uewelewa huthubutu kutembelea wizara yao husika ya Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) ili waweze kupata miongozo na maboresho mbalimbali ambayo yangeweza kuwasaidia katika uongozi wao," anasema.
Suala lingine walilolibaini ni kuwa katika baadhi ya vijiji havina kamati za mipango shirikishi na kutolea mfano wa vijiji hivyo ni kijiji cha Malumbo.
Anasema kuwa hiyo ni kutokana na utendaji mbovu wa kiongozi wao mkuu, kwasababu vitu hivyo vipo wazi kwamba lazima ruzuku za maendeleo zipitie katika kamati hiyo.
"Hali hii imesababisha tuone kwamba elimu hii ya
uraia itolewe kwa uhumimu na isihubiri tu wakati wa
kupiga kura, jamii inatakiwa ijengewe uwezo wa kutambua nini maana ya elimu ya uraia ambayo itasaidia katika kuchagua viongozi wao," anasema Bw.Silumbi.
Anaongeza kuwa "Ni vyema Tamisemi ianze kuchukua jitihada za dhati ili kuwasaidia wananchi wengi wa chini ili waweze kutoka hapa walipo na waweze kupata maendeleo yenye tija, kwani utawala bora ni nguzo ya maendeleo".
Diwani wa Kata ya Malumbo, Bw.Salehe Kinyogoli akizungumzia suala la utawala bora katika kata yake anasema ni jambo la kuzingatiwa ili wananchi waweze kupata maendeleo.
Bw.Kinyogoli anasema kiongozi wa serikali ya kijiji anatakiwa kufuata misingi ya utawala bora kama ilivyowekwa ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika utekelezaji wa majukumu yake.
"Kiongozi anayejua majukumu yake hayumbishwi, anakua
hana upendeleo na anawajibika ipasavyo kwa wale anaowaongoza," anasema Bw.Silumbi.
Anasema, Mwenyekiti wa kijiji anatakiwa kuitisha mkutano katika kijiji chake kila baada ya miezi mitatu ili kuzungumza na wananchi wake kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.
Anasema kuwa hata hivyo, suala hilo limekuwa tatizo kwa baadhi ya viongozi hao kwa kuogopa kuhojiwa na wananchi kuhusu masuala ya mapato na matumizi ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya vijiji husika.
"Kiongozi wa kijiji kukataa kuitisha mikutano ya wananchi unajitia mashaka kwa wananchi wako, utaonekana mwizi, kwanini ukatae mkutano, ni vyema mkaitisha mikutano ili muwape wananchi nafasi ya kutoa madukuduku yao," anasema Bw.Kinyogoli.
Anasema, kamati ya ulinzi na usalama hazitekelezi majukumu yao vizuri kwakuwa kuna baadhi wya vijana katika kata hiyo wamekuwa wakifanya vitendo vya uhalifu kama kuvuta bangi hadharani na hawachukuliwi hatua.
Hata hivyo suala hilo linapingwa vikali na mjumbe wa
kamati ya uadilifu katika kijiji cha Malumbo Bi.Aisha Kikando na kusema kuwa wamekuwa wakiwakamata vijana hao lakini mwenyekiti wao hawachukulii hatua zinazostahili.
Bi.Kikando anasema kuwa wanapowakamata vijana hao huwapeleka katika ofisi ya Mtendaji wa kijiji na huko hulipishwa faini ya shilingi 10,000 bila risiti na haijulikani fedha hizo zinapokwenda.
Anasema kuwa hatua hiyo imefanya vijana wengi
kuendelea na vitendo hivyo jambo ambalo limekuwa
likituvunja nguvu utendaji wa kamati yao.
Naye Bi.Aisha Mwinyimkuu ambaye ni mjumbe wa kamati
ya uadilifu katika Kijiji cha Kidugaro cha Kanga
anasema katika kijiji chao suala la utawala bora
lina mapungufu mengi ikiwemo wananchi kutopenda
kuhudhuria mikutano ya maendeleo inapoitishwa.
Bi.Mwinyimkuu anasema mikutano inapoitishwa, wananchi
huona kama wanasumbuliwa na kudai kuwa viongozi wao
hawana jipya la kuwaeleza.
Bw.Ally Lubawa kutoka kijiji cha Palaka anasema
viongozi wa kijiji chao wanajitahidi kushirikisha
wananchi katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano.
Anasema kuwa hivi karibuni, katika kijiji chao kulikuwa na mwekezaji mzungu aliyechukua eneo kwa ajili ya shamba na kilimo zao la Miyemba ambapo viongozi wa kijiji hicho waliwashirikisha wananchi kabla ya uwekezaji.
Anasema kuwa Juni mwaka huu ilikuwa mara ya mwisho kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho kufanya mkutano wa maendeleo na wananchi.
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Palaka Bw.Zuberi Kikombe anasema kutokuwepo kwa utawala bora vijijini kunachangiwa na viongozi wa vijiji kutopewa semina za uongozi pale wanapochaguliwa.
Hali hiyo inasababisha baadhi yao kutotambua wajibu wao hivyo hufanya kazi kwa uzoefu.
Bw.Kikombe anasema katika kijiji chake kuna vikundi vya ulimaji wa ufuta pamoja na kufuga mbuzi ambavyo hata hivyo vinalegalega kutokana na kutopata msukumo.
Anasema kuwa kwa sasa wana mpango wa kilimo ambapo
jumla ya wanavijiji 380 wamepewa hekari tano za shamba
kila mmoja.
Katika hatua nyingine, Bw.Kikombe amelishukuru shirika la PADA kwa kutoa elimu ya utawala bora hasa maeneo ya vijijini kwani imewaamsha kujua majukumu yao kwa wananchi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment