11 September 2012

SBL yatoa msaada wa vifaa kwa Polisi


Rehema Maigala na Rose Itono

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL), imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni 17.5, kwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ili viweze kutumika katika wiki ya nenda kwa usalama barabarani inayoanza Septemba 17 mwaka huu.

Akikabidhi vifaa hivyo Dar es Salaam jana kwa Kamanda wa kikosi hicho, Mohamed Mpinga, Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo Bi. Teddy Mapunda, alisema SLB imeona umuhimu wa kuchangia operesheni hiyo kutokana na umuhimu wake nchini.

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni fulana na bampa stika ambazo zimebeba ujumbe wa kauli mbiu ya wiki hiyo mwaka huu inayosema, “Pambana na ajali mbalimbali za barabarani
kwa vitendo, zingatia sheria”.

Akipokea vifaa hivyo, Kamanda Mpinga alishukuru kampuni hiyo kwa msaada waliotoa na kufafanua kuwa maadhimisho hayo kitafifa, mwaka huu yatafanyika mkoani Iringa.

Alisema katika wiki hiyo, shughuli mbalimbali zitafanyika pamoja na kutoa mafunzo kwa waendesha pikipiki zaidi ya 500 nchini, vyeti kwa washiriki na leseni.

“Tumeamua kutoa mafunzo hayo kwa waendesha pikipiki kutokana na idadi kubwa ya ajali zinazochangiwa na ukiukwaji sheria, uvaaji kofia ngumu na upakiaji zaidi ya mtu mmoja,” alisema.

Aliwasihi waendesha pikipiki kuheshimu alama za usalama barabarani, sheria na kuacha kufanya maandamano inapotokea ajali ya mwendesha pikipiki.

No comments:

Post a Comment