11 September 2012

Prof. Lipumba: Serikali haipo makini


Na Anneth Kagenda

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Watanzania wanaokosa huduma za kijamii kama matibabu na umaskini uliokidhiri unatokana na ukosefu wa Serikali makini isiyowajali.


Prof. Lipumba aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika uzinduzi wa Operesheni Mchakamchaka hadi 2015, iliyofanyika katika Viwanja vya Jangwani.

Alisema ni wazi kuwa Serikali iliyopo madarakani haina huruma na wananchi wake ndio maana inashindwa kutekeleza mambo muhimu wakati kuna rasirimali za kutosha kama gesi, madini na bahari.

Akizungumzia mgawo wa umeme, alisema wananchi wamekuwa wakidanganywa kwamba mgawo haupo wakati upo ndio maana unakatika mara kwa mara au siku nzima.

“Nakumbuka Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema utafika wakati tutaondokana na tatizo hili lakini jambo la kushangaza mgawo upo hadi leo, Serikali yake haipo makini,” alisema.

Aliwataka wananchi wahakikishe Katiba Mpya inaweka wazi kipengele cha Watanzania kunufaika na raslimali zilizopo.

“Ili kuhakikisha Watanzania wanaondokana na changamoto walizonazo ni vyema Serikali iwape fedha mikononi kwani zipo baadhi ya nchi ambazo zinatumia mfumo huu kuboresha maisha ya wananchi wake.

“Umaskini ni tatizo kubwa kwenye nchi yetu, kama Serikali ingetoa fedha kwa wananchi wake mkononi, wangeweza kufanya mambo ya msingi kama biashara ili kujipatia kipato cha uhakika,” alisema.

Aliongeza kuwa, kama CUF itapewa ridhaa ya kuongoza nchi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, ina malengo mazuri kwa wananchi hususan vijana ambao wanashindwa kupewa kazi viwandani badala yake wanakaa mitaani na kuwa ombaomba.

Prof. Lipumba vhama hicho kikiunda Serikali, jambo hilo ni dogo kwao hivyo ni wajibu wa wananchi kuwapa ridhaa ya kuongoza nchi ambapo hivi sasa Serikali imekuwa bingwa wa kutoa misamaha ya kodi.

Aliongeza kuwa, bei za bidhaa na vyakula kama maharage, mchele, mahindi, ufuta, alizeti, karanga vimepanda kwa bei ya kutisha kutokana na uchumi kubadilika ambapo sera ya CCM inayohusu Kilimo Kwanza haimlengi mkulima wa kipato cha chini.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Bw. Julius Mtatiro, alisema CCM wameshindwa kuongoza nchi na sasa wameanza kuua wananchi wake huku wakizunguka na kusema hicho cha Waislamu jambo ambalo halina ukweli wowote.

“CCM wanasema sisi na wao ni mapacha, mbona makada wao wamekuwa wakipeleka misaada kwa CHADEMA na hao tuwaite watoto wake, jambo la msingi wakubali kwamba nchi imewashinda  si vinginevyo,” alisema Bw. Mtatiro.

No comments:

Post a Comment