07 September 2012
Saintfiet ajivunia ubora wa kikosi cha Yanga
Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa Yanga Mbelgiji Tom Saintfiet amesema kuwa siku zinavyozidi kwenda ndivyo kikosi chake kinavyozidi kuimarika na hivyo kumpa matumaini makubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ligi Kuu inaanza kutimua vumbi Septemba 15, mwaka huu ambapo Yanga wataanza kwa kucheza na Prisons ya Mbeya iliyopanda daraja msimu huu, mechi hiyo imepangwa kufanyikia Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha huyo alisema kikosi chake si kibaya kwani wachezaji wamekuwa wakifanya mazoezi kwa kujituma na kila mmoja anaonesha uwezo wake binafsi hali ambayo inamtia matumaini.
"Timu yangu ipo vizuri, kwani wachezaji wanacheza kwa kuelewana tofauti na awali walikuwa hawajuani, hivyo kwa sasa tupo tayari kwa Ligi Kuu itakayoanza wiki ijayo," alisema Tom.
Alisema wachezaji wake majeruhi sasa hivi wameanza mazoezi ambao ni kipa Yaw Berko, ambaye kwa sasa yupo fiti na kiungo Nurdin Bakari naye hali yake si mbaya.
Tom alisema lengo lake kubwa ni kuona timu hiyo inatwaa ubingwa msimu huu kama walivyofanya katika michuano ya Kombe la Kagame, kwani anaamini mashabiki wao bado wanahamu na vikombe katika klabu yao.
"Hakuna kocha ambaye anafurahia kama kutwaa kombe, kwani ni fafari kubwa sana hivyo na mimi nataka kuandika historia kwa kutwaa makombe zaidi katika timu yangu hii mpya," alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment