07 September 2012

Simba yanywea kwa 'Paka' U/Taifa *Daniel Akuffor Azimia uwanjani wakipigwa 3-0


Na Victor Mkumbo

MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba jana walikuwa wadogo mbele timu ya Sofapaka ya Kenya, baada ya kuzabwa mabao 3-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuwafanya mashabiki wake waliojitokeza kwa shauku kubwa ya kuwaona wachezaji wao wapya wakifanya vitu vyao wakitoka vichwa chini uwanjani.

Hata hivyo katika mechi hiyo dakika ya 34, mchezaji wa kimataifa wa Simba raia wa Ghana Daniel Akuffor, alipoteza fahamu baada ya kugongana na mabeki wa Sofapaka na kulazimika kutolewa ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Abdallah Juma.

Sofapaka ilianza kushangilia bao lake la kwanza dakika ya 18, lililofungwa kwa mkwaju wa penalti uliokwamishwa wavuni na John Baraza, baada ya beki wa Simba Kobel Keita, kuunawa mpira akiwa katika harakati za kuokoa hatari langoni mwake kutokana na mpira wa kona uliopigwa na Obson Monday.

Awali Simba iliingia uwanjani kwa nguvu ambapo dakika ya pili ilipeleka shambulizi la nguvu langoni mwa Sofapaka, ambapo Akuffor aliachia shuti kali la mbali baada ya kupokea pasi ya Salum Kinje, lakini mpira ulitoka nje kidoga ya lango.

Dakika ya tano Sofapaka ilijibu shambulizi hilo ambapo, Baraza nusura aifungie timu yake bao lakini, beki wa Simba Keita akamzidi mbio mshambuliaji huyo na kuokoa hatari hiyo.

Katika kipindi hicho cha kwanza Sofapaka, walipeleka mashambuzi mengi langoni mwa Simba, ambayo ilionekana kupoteana lakini washambuliaji wake hawakuwa makini katika kukwamisha mpira wavuni.

Mshambuliaji chipukizi wa Simba, Christopher Edward dakika ya 45 alishindwa kuipatia bao timu yake baada ya kuunganisha krosi iliyochongwa na Mrisho Ngassa ambapo mpira ulitoka nje.

Kipindi cha pili Simba ilianza kwa kasi ambapo dakika ya 47 Ramadhan Chombo 'Redondo', nusura aipatie timu yake bao lakini shuti lake likatolewa nje na beki wa Sofapaka na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya 56, Sofapaka iliandika bao la pili lililowekwa kimiani na Baraza, kwa shuti kali lililomshinda Juma Kaseja, aliyeambulia kupeta bila mafanikio.

Baada ya bao hilo la pili, Simba ilipoteana na kuwaachia nafasi Sofapaka kutanuwa wanavyotaka uwanjani na ambayo ilipata bao la tatu dakika ya 66 lililofungwa na Joseph Nijaga, aliyeunganisha krosi ya Baraza ambaye alitumia nafasi ya wachezaji wa Simba ambao waloikuwa wakicheza bora liende.

No comments:

Post a Comment