12 September 2012

SACCOS yaomba kufikishiwa umeme wajikomboe kiuchumi



Na Mercy James, Mbarali

CHAMA cha Akiba na Mikopo cha Madibira SACCOS, kilichopo Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, kimeiomba Serikali iwafikishie nishati ya umeme wa gridi ya Taifa, waondokane na kero ya kutumia mashine zinazotumia mafuta ya dizeli kukoboa mpunga wanaolima.


Wanachama wa SACCOS hiyo waliyasema hayo jana wakati wakizungumza na gazeti hili baada ya kupatiwa mafunzo ya kibenki na watalamu kutoka Benki ya CRDB mjini Njombe, mkoani Iringa.

Walisema ukosefu wa nishati hiyo, unawafanya washindwe kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya kilimo kutokana na fedha nyingi kutumika kwa kununulia mafuta ya dizeli.

Waliongeza kuwa, licha ya kulima mpunga kwa wingi, ukosefu wa nishati ya umeme unakwamisha malengo waliyonayo ili kuboresha maisha yao.

Kaimu Meneja wa SACCOS hiyo, Bw. Henry Mdapo, alisema chama hicho kimenunua kinu cha kisasa lakini miundombinu imara inakwamisha maendeleo ya wanachama wao.

Alisema wakulima hulazimika kusafirisha mazao yao baada ya kuvuna na wale wasio na mtaji mkubwa, hukoboa katika mashine zao ambazo hutumia mafuta ambayo garama yake ni kubwa hivyo wanashindwa kuziendesha na kulazimika kuuza mpunga usiokoolewa.

“Kwa muda mrefu tumeahidiwa na viongozi kuletewa umeme wa gridi ya Taifa lakini utekelezaji wake ni mgumu kama walivyoahidi hatuelewi ni lini tutaondokana na adha hii,” alisema mwanachama wa SACCOS hiyo, Bw. Said Kilawa.

Naye Bi. Rehema Njuyu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa SACCOS hiyo, aliwataka wanawake kuona umuhimu wa kukopa na kuacha woga ili waweze kuendesha shughuli za kilimo.

Kwa upande wake, Bw. Bruno Teodory aliwataka wanchama hao kuutumia umoja wao ili kushirikiana na benki hiyo waweze kujikomboa kiuchumi na kuboresha maisha yao.

No comments:

Post a Comment