12 September 2012

Lipo la kujifunza maandamano ya waandishi



WAANDISHI wa habari kutoka mikoa mbalimbali nchini, jana walifanya maandamano ya amani kulaani mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi.


Inaelezwa kuwa, mauaji ya Mwangosi, yalitokana bomu ambalo lilipigwa na polisi Septemba 2 mwaka huu, katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, kwenye vurugu zilizohusisha wafuasi wa CHADEMA na polisi.

Kutokana na mauaji hayo, waandishi wa habari kupitia vyama vyao (Press Club), katika mikoa mbalimbali, walitoa matamko ya kulaani mauaji ya kikatili dhidi ya mwanahabari mwenzao sambamba na kususia kazi za jeshi hilo kwa kipindi kisichojulikana.

Pamoja na Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kuunda kamati ya kuchunguza mauaji hayo, Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), lilitoa tamko la kuwataka waandishi kufanya maandamano ya amani nchi nzima.

Katika maandamano yaliyofanyika jana, waandishi walishika mabango yaliyokuwa na ujumbe tofauti. Baadhi ya mabango yalisisitiza umuhimu wa askari wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo kuchukuliwa hatua pamoja na Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kama inavyofanyika kwa watumishi wengine.

Waandishi wa habari wanaamini kuwa, Kamanda Kamuhanda, alishindwa kuokoa maisha ya Mwangosi kabla ya kuuawa akiwa eneo la tukio bila kutoa msaada wowote.

Sisi tunasema kuwa, maandamano hayo yana ujumbe mzito kwa Serikali ambayo haiwezi kutekeleza mikakati yake ya maendeleo bila kushirikisha vyombo vya habari.

Ni wazi kuwa, mauaji ya Mwangosi yameibua uhasama kati ya Jeshi la Polisi, Serikali na waandishi ambao kalamu zao zina nguvu kubwa
ya kuchochea maendeleo, machafuko na kuimarisha amani iliyopo.

Umefika wakati wa Serikali na Jeshi la Polisi kutafuta namna bora ya kurudisha uhusiano ulioanza kupotea kati yao na waandishi sambamba na kuhakikisha askari waliohusika na mauaji hayo wanachukuliwa hatua bila kujali nafasi zao.

Kitendo cha waandishi wa habari katika baadhi ya mikoa nchini kukataliwa kuandamana kwa madai ya kuchelewa kutoa taarifa za maandamano hatukiungi mkono kwani kimewanyika haki yao ya msingi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kama tofauti zilizojitokeza kati ya Serikali, Jeshi la Polisi na waandishi hazitapatiwa ufumbuzi wa haraka, upo uwezekano mikaakati mbalimbali ya Serikali kwa wananchi wake kukwama kwani vyombo vya habari ndio daraja la maendeleo kati ya wananchi na watawala.

No comments:

Post a Comment