07 September 2012

Redds Miss Ilala kufanyika leo, zawadi zatangazwa



Na Amina Athumani

MSHINDI wa mashindano ya Urembo la Redd's Miss Ilala 2012 anatarajia kunyakua kitita cha sh. milioni 1.5 , katika kinyang'anyiro kitakachofanyika leo katika ukumbi wa Nyumbani Lounge, Dar es Salaam.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa mashindano hayo Juma Mabakila alisema mrembo huyo atakata tiketi ya kushiriki Redd's Miss Tanzania 2012 litakalofanyika baadae mwaka huu.

Alisema mrembo huyo ambaye atakuwa mrithi wa Salha Israel ambaye ni Miss Tanzania mwaka 2012, wanaimani kwa mwaka huu pia mshindi wa Tanzania atatokea Ilala.

Alisema zawadi ya mshindi wa pili atapata sh. milioni 1.2, wa tatu ataondoka na sh. 700,000, wa nne hadi wa tano sh. 400,000 kila mmoja na washiriki waliobakia kila mmoja atapata  kifuta jasho cha sh. 200,000.

Alisema onesho hilo litapambwa na burudani kutoka B Band watakaoshirikiana vema na machozi Band, Chege Chigunda, Banana Zoro, Ommy Dimpoz na Lady Jay Dee.

Alisema wasanii hao watatumia bendi katika kuonesha umahiri wao wamejumuika kwenye onesho hilo ili kukidhi kiu ya mashabiki wa urembo.

Alisema pia Msanii wa filamu Steve Nyerere atalipamba jukwaa kama MC wa shughuli hiyo ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa.

Alisema shindano hilo litaoneshwa moja kwa moja kupitia mtandao wa Uhuru One, ili kila Mtanzania atakayekosa kufika ukumbini kulishuhudia moja kwa moja.

Alisema kamati ya Miss Ilala imezingatia mchango wa wadhamini kwa matangazo yao kuonekana nje ya mipaka ya jiji la Dar es  Salaam na nje ya hapo.

Warembo 14 watakaowania taji hilo ni Mary Chizi, Matilda Martin, Magdalena Mnisi, Suzan Deodats, Whitness Michael, Stella Moris na Elizabeth Petty.

Wengine ni Willimina Mvungi, Zawadi Mwambe, Rehema Said, Diana Simon, Amina Sangwe, Noela Michael, Phillios Lemi.

Miss Ilala ina rekodi ya kutoa warembo wa nne waliotwaa taji la Miss Tanzania mwaka 1999 ni Hoyce Teme, 2002 Jaclyne Ntuyabaliwe, 2002 Angela Damasi na 2011 Salha Israel anayeshikilia taji hilo kwa sasa ambapo kwa mwaka huu imepania kuendeleza kutwaa hilo.

No comments:

Post a Comment