11 September 2012

Meli iliyoruka foleni bandarini yalalamikiwa



Na Mwandishi Wetu

WAFANYABIASHARA wa mafuta nchini, wamelalamikia hatua ya meli moja kuruka foleni na kwenda kupakua shehena ya mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.


Hatua hiyo imeanza kuibua msuguano kwa wafanyabiashara ambao wanadai kitendo hicho hakiwezekani ambapo kutokana na hali hiyo, Umoja wa Kampuni za Mafuta (OMC) umeandika barua kwenda Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kuilalamikia Kampuni ya Kuratibu Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PIC).

Chanzo cha mgogoro huo ni baada ya PIC kuruhusu meli hiyo ambayo imebeba shehena ya mafuta ya MT Atlantic Diana, kupakua kwenye Bomba la Mafuta Kurasini (KOJ 1) wakati awali iliruhusiwa kushusha kwenye KOJ 2, ikidaiwa imebeba shehena ya mafuta ya ndege.

Katika maombi yake, wafanyabiashara waliobeba shehena hiyo waliomba kushusha shehena hiyo katika bomba la KOJ 2, wakidaia ni mafuta ya ndege na ambayo shehena yake inakaribia kuisha.

Kupitia barua hiyo, umoja wa kampuni za mafuta unalalamikia uamuzi uliofanywa na PIC kuwa umesababisha ucheleweshaji wa baadhi ya meli kuendelea kubaki kwenye foleni hivyo kulipa gharama za kusubiri kupakua shehena melini.

Wafanyabiashara hao wanalalamikia uamuzi wa kutoa zabuni ya dharura ya kuagiza mafuta ya ndege wakati kuna shehena ya kutosha kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Zabuni hiyo ilitolewa kwa Kampuni ya Augusta Energy SA kwa masharti ya kushusha shehena yake kupitia bomba la KOJ 2 ili kutoingilia mlolongo wa kupakua mafuta kwenye KOJ 1.

Hivi karibuni, Kampuni ya Augusta Energy ilishindwa zabuni ya kuagiza mafuta chini ya mfumo wa BPS, kabla ya hapo kampuni hiyo ilikuwa ikiagiza mafuta chini ya mfumo huo kuanzia Januari mwaka huu.

“Tunaiomba EWURA iingilie kati sakata hili kwani hatua hiyo imetusababishia hasara ambayo itavuruga upangaji wa bei elekezi ya kipindi kijacho,” walisema.

No comments:

Post a Comment