10 September 2012

Padri Mapunda atema cheche *Awavaa viongozi wa dini kwa kujaa woga *Ahoji ukimya wao kukemea maovu yaliyopo



Na Anneth Kagenda

PADRI wa Kanisa Katoliki, Baptiste Mapunda na Mkurugenzi wa Shirika la Farijika la Afrika Mashariki, amewashukia viongozi wa dini nchini, wakiwemo maaskofu, wachungaji na mapadri wenzake, kwa kukaa kimya na kushindwa kukemea maovu yanayotendeka.


Alisema kama sababu ya kushindwa kufanya hivyo inatokana na woga, wanapaswa kubadilika kwani viongozi wote wa dini walipakwa mafuta kwa ajili ya kuhubiria Taifa.

Padri Mapunda aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki, Usharika wa Kongowe.

“Kwanini wakae kimya...viongozi wengi wa dini wakiwemo maaskofu wanazungumzia fedha wakati ekalu chafu, kwanza wafanye mambo yanayompendeza Mungu.

“Wakatoliki ni viziwi, wanaogopa kusema, mimi siwezi kukaa kimya nimeshindiliwa na roho wa Mungu, hakuna sababu ya kuogopa kusema ukweli ili usiuawe,” alisema.

Baada ya kusema hayo, Padri Mapunda aliwageukia polisi na kusema wakati umefika kwa jeshi hilo, kuacha kuwanyanyasa watu, kwani nchi zingine za Ulaya, polisi ndio kimbilio la raia.

“Polisi wetu msigeuze Tanzania kama Bukinafaso...Tanzania sio kisiwa cha mabomu,” alisema na kusisitiza kuwa, mauaji ya mwandishi wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, kimelitia doa jeshi hilo.

“Unamuua mwandishi wa habari, huku ni kuua uhuru wa habari,” alisema na kudai kushangazwa na hatua ya Serikali kuonekana ipo likizo na kukimbilia kuunda tume.

“Kuunda Tume ni ubabaishaji, kama Serikali imeshindwa kuchukua hatua, mawaziri wajiuzulu, kitendo cha kuuawa Mwangosi tena kikatili ni kielelezo kuwa Tanzania imefikia pabaya,” alisema.

Alisema askari waliofanya mauaji hayo, waumbuliwe hapa duniani, ambapo Mawaziri wanaoendeleza maovu, wataunguzwa moto.

Aliongeza kuwa, uhuru wa Tanzania ulipatikana bila kumwaga damu hivyo inashangaza baada ya miaka 50, vitendo hivyo vimeanza tena kwa kasi ya ajabu.

Alisema awali kulikuwa na siasa za kidemokrasia lakini hivi sasa mfumo huo umeondolewa na kuja siasa za rushwa na ufisadi.

No comments:

Post a Comment