05 September 2012

OSHA yataka waajiri watoe ushirikiano


Tumaini Maduhu na David John

WAAJIRI nchini wametakiwa kushirikiana na Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), ili kutoa elimu ya usalama ambayo itasaidia kupunguza ajali zinazotokea sehemu za kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa OSHA, Bi. Akwilina Kayumba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mafunzo yalihusisha wafanyakazi kutoka sekta zote nchini.

Alisema OSHA imekuwa ikiandaa mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wa sekta zote nchini ili kuwajengea uwezo na uzoefu ambao utawasaidia kufahmu na kuzingatia taratibu za usalama mahali pa kazi ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea.

Aliongeza kuwa, wao kama wakala wamekuwa wakipambana na baadhi ya waajiri wasiotaka kuboresha huduma za afya katika maeneo ya kazi.

“Sisi kama wakala, tumekuwa tukitoa adhabu kwa baadhi ya waajiri ambao hawazingatii huduma mahali pa kazi kwa kuwatoza faini au kuwanyang'anya leseni ili kuboresha huduma za afya mahali pakazi,” alisema Bi. Kayumba.

Alisema ili kuhakikisha huduma za afya zinakuwepo mahali pa kazi, wameweka mitandao ambayo inawasaidia wafanyakazi kutoa malalamikoa yao.

Bw. Kayumba alisema licha ya kuboresha huduma za afya mahali pa kazi, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo waajiri kutokuwa na mwamko wa kupeleka wafanyakazi katika mafunzo ya muda mrefu.

“Hili ni tatizo ambalo tunakabiliana nalo lakini tunawaelimisha waajiri wahakikishe wafanyakazi wao wanapata elimu ambayo tunaamini itaboresha huduma ya afya mahali pa kazi,” alisema.


No comments:

Post a Comment