05 September 2012
Jamii ifuatilie matumizi fedha za ruzuku - MPR
Na Stella Aron
WITO umetolewa kwa wananchi kujenga tabia ya kufuatilia matumizi ya ruzuku zinazotolewa na Serikali wilayani ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yanayokusudiwa.
Ushauri huo umetolewa na hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na Harakati Kupunguza Umaskini (MPR), Bw. Godfrey Kafuru, katika mafunzo ya ufuatiliaji wa matumizi ya ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya maji, Kata ya Kibamba na Mbezi.
Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na MPR, yamefadhiliwa na Shirika la Foundation For Civil Society, ambapo Bw. Kafuru aliongeza kuwa, lengo ni kuhakikisha jamii inachukua fursa ya kuitambu taasisi hiyo na kufahamu wajibu na haki zao katika kufuatilia fedha za ruzuku zilizotengwa kwa ajili ya huduma.
“Sababu za kuanzishwa taasisi hii ni nyingi lakini kubwa zaidi ni jamii kukabiliwa na changamoto nyingi hasa zinazotuhu tatizo la upatikanaji wa maji,” alisema.
Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo Bw. Mngojo Bakari, alisema mafunzo hayo yamegawanyika sehemu nne ambazo ni mbinu za ufuatiliaji wa fedha za ruzuku, kuunda kamati za ufuatiliaji wa fedha za rukuzu katika sekta ya maji Kibamba na Mbezi, kutathmini mafanikio na matatizo ya utekelezaji wa mradi huo.
Alisema tatizo la maji katika kata hiyo ni la muda mrefu hivyo uwepo wa kamati ambazo zitakuwa zikifuatilia ruzuku hizo, itasaidia kufanikisha uchimbaji visima katika baadhi ya maeneo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo Bw. Thomas Monsi, aliwataka washiriki kuzingatia mafunzo hayo ili wawe na nyenzo ambazo watazitumia kufuatilia matumizi ya fedha hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment