05 September 2012
Afariki dunia katika nyumba ya wageni Dar
Lulu Malenda na Jesca Kileo
WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti jijini Dar es Salaam, likiwemo la mkazi wa eneo la Moshi Bar, Ukonga, Hamad Ali Hamad (36), ambaye ni fundi magari.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Komba, alisema tukio la kwanza lilitokea Septemba 2 mwaka huu, ambapo mwili wa Hamad ulikutwa kitandani akiwa amekufa katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Blue Victoria iliyopo Buguruni Rozana.
“Mwili huu haukuwa na jeraha lolote na ulikutwa katika chumba namba nane, uchunguzi wa awali umebaini marehemu alifika katika nyumba hiyo Septemba mosi.
“Alijiandikisha kwa jina la Ernest Abdalah, lakini baada ya mwili wake kupekuliwa, alikutwa na kitambulisho cha kura chenye jina la Hamad, fedha taslimu sh. 22,850 na simu ya mkononi aina ya Nokia,” alisema Kamanda Komba.
Alisema mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na upelelezi wa tukio hilo unaendelea.
Katika tukio lingine, mkazi wa Rombo mkoani Kilimanjaro Sebastian Wiliam Kimaro (34), amedondoka ghafla na kufa papo hapo ambapo tukio hilo limetokea Septemba 2 mwaka huu eneo la Buguruni Relini.
Kamanda Komba alisema, Kimaro alifariki baada ya kutoka kwenye kilabu cha pombe za kienyeji na uchunguzi wa awali ulibaini wakati wa uhai wake alikuwa akiugua ugojwa wa Kifua Kikuu (TB).
Baada ya kupekuliwa alikutwa na vyeti vya Hospitali ya Kibogoto, iliyopo Wilaya ya Hai, vikionesha alikuwa na ugonjwa huo. Mwili wake umehifadiwa Hospitali ya Amana na upelelezi unaendelea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment