10 September 2012

Okwi, Kiiza watulizwa Zambia



NDOLA, Zambia

WASHAMBULIAJI wa timu ya Taifa ya Uganda 'The cranes', Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza, wameshindwa kutakata kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia baada ya kushuhudia timu yao ikichapwa bao 1-0 na mabingwa wa Afrika, Zambia 'Chipolopolo'.

Wachezaji hao wanacheza soka la kulipwa Tanzania katika timu za Yanga na Simba ambapo timu hizo zilikutana juzi katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika, mwakani.

Kwa mujibu wa mtandao wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ulieleza kwamba bao hilo pekee la Zambia  lilifungwa na nahodha,  Christopher Katongo katika dakika ya 17 na kuifanya timu yake itoke kifua mbele nyumbani.

Katongo ambaye anacheza soka la kulipwa, China alitumia vizuri uzembe wa mabaeki wa Uganda na kufunga bao hilo akipokea pasi nzuri ya Davies Nkausu na kuwafanya mashabiki 40,000 waliokuwepo uwanjani hapo kushangilia kwa nguvu.

Uganda iliyoongozwa na Okwi na Kiiza, walishindwa kuonesha cheche zao baada ya kukutana na ukuta imara wa Zambia ambapo pia timu yao inasaka nafasi ya kushiriki michuano hiyo kwa mara nyingine baada ya kucheza mwaka 1978 ambapo ilitumia muda mwingi 'kupaki basi' hali iliyowafanya wasitengeneze nafasi nyingi za kufunga.

Katika mechi hiyo, Uganda ilikosa nafasi moja ya wazi kupitia kwa mchezaji aliyeingia, Dan Wagaruka aliyepiga shuti kali lakini liliokolewa na kipa wa Zambia, Kennedy Mweene na kuwa kona tasa.

Timu hizo zitakutana tena mwezi ujao kwenye Uwanja wa Nambole jijini Kampala, Uganda katika mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani kutokana na kila timu kusaka nafasi ya kucheza michuano hiyo itakayofanyika Afrika Kusini katika majiji ya Johannesburg, Durban, Port Elizabeth, Nelspruit na Rustenburg.

Katika mechi zingine zilizochezwa juzi, Ghana iliichapa Malawi mabao 2-0 ambapo mabao yao yalifungwa na Christian Atsu na Anthony Annan na Afrika ya Kati iliichapa Burkina Faso bao 1-0 kwa bao lililofungwa na Vianney Mabide.

Nayo timu ya Ivory Coast ilitoka nyuma na kuichapa Senegal mabao 4-2 kwa mabao ya Salomon Kalou, Gervinho, Didier Drogba na Max Gradel huku ya Senegal yakifungwa na Dame Ndoye na Papiss Cisse.

Matokeo mengine ya mechi hizo ni kama ifuatavyo:
 Gabon 1-0 Togo
 Sierra Leone 2-2 Tunisia
 Mali 3-0 Botswana
 Cape Verde 2-0 Cameroon
 Sudan 5-3 Ethiopia
  Liberia 2-2 Nigeria

No comments:

Post a Comment