24 September 2012
NEC yaanza maandazi uchaguzi wa madiwani
Na Rose Itono
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeanza maandalizi ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 29 zilizopo katika halmashauri 27, Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa NEC Taifa, Jaji mstaafu Damian Lubuva, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa maandalizi ya chaguzi hizo ambao ulihudhuriwa na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini.
Alisema uchaguzi huo utafanyika Oktoba 28 mwaka huu ambapo NEC imejiandaa kuhakikisha shughuli zilizoainishwa katika ratiba zitafanyika kwa muda uliopangwa ili kuhakikisha kila mtu mwenye sifa anashiriki kuchagua kiongozi anayemtaka.
“NEC imekusudia kuhakikisha chaguzi hizi zinafanyika kwa uwazi, uhuru na haki kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kujenga demokrasia na kuimarisha utawala bora,” alisema.
Jaji Lubuva aliongeza kuwa, NEC itafikisha vifaa vya uchaguzi katika maeneo husika kwa muda uliopangwa ili kupunguza usumbufu kwa wapiga kura.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NEC, Bw. Julius Mallaba, alisema uteuzi wa wagombea utafanyika Oktoba 2 mwaka huu na kampeni zitaanza Oktoba 3 hadi 27 mwaka huu.
“Fomu za uteuzi wa wagombea zimeanza kutolewa na wasimamizi wa uchaguzi hadi Oktoba 2 mwaka huu, tayari NEC imeteua watendaji ambao watasimamia chaguzi hizi.
“Hivi sasa tunaendelea na maandalizi mengine ambayo ni kutoa mafunzo kwa watendaji, uchapishaji na ununuzi wa vifaa vya uchaguzi pamoja na orodha za majina ya wapiga kura,” alisema.
Alivitaka vyama ambavyo vitashiriki chaguzi hizo kuwasilisha orodha ya mawakala wao kwa msimamizi wa uchaguzi ikionesha majina yao na vituo walivyopangiwa siku saba kabla ya uchaguzi.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambao walihudhuria mkutano huo, walitoa maoni yao kwa NEC ili uchaguzi huo uwe wa haki.
Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Msafiri Mtemelwa, alisema haoni sababu ya kuwa na tume inayowatumia Wakurugenzi kama wasimamizi wa uchaguzi bila kuwa na mtandao kutoka nje.
“Wakurugenzi wa NEC ni makada wa CCM hivyo ni vigumu kuwa na uchaguzi huru, lazima kuwe na mtandao, upo umuhimu wa tume kuijenga safu yake katika misingi inayokubalika.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha UDP, Bw. Issac Cheyo, alisema daftari la uchaguzi lina mkanganyiko na kuitaka NEC Kujenga ushirikiano na vyama vya siasa ili kurekebisha kasoro.
Bw. Emanuel Makaidi kutoka Chama cha NLD, alisema hakuna uchaguzi uliofanya madudu kama wa mwaka 2010, ndiyo maana una kesi nyingi ambazo hadi sasa zimefunguliwa 47.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment