24 September 2012

CHADEMA kuhamasisha maandamano Iringa



Na Eliasa Ally, Iringa

MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), ameahidi kuhamasisha maandamano kwa wakazi wa Mkoa huo kesho ili Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, aweze kuhamishiwa kituo kingine cha kazi.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini humo jana, Mchungaji Msigwa alisema uamuzi huo unatokana na Kamanda Kamuhanda kushindwa kuwajibika baada ya kutokea mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona kiongozi ambaye alishindwa kuwalinda waandishi wa habari wakiwa kazini na kusababisha mauaji akiendelea kuvaa gwanda na kuingia ofisini.

“Kila wiki tutakuwa na maandamano kuhakikisha Kamanda Kamuhanda anatoka katika Mkoa huu, ametukuta tukiishi kwa amani kwani ni ajabu kuona mtu aliyesababisha mauaji, akiendelea  kulinda usalama wa Mkoa,” alisema.

Aliongeza kuwa, yeye ataendelea kufanya kazi na vyombo vya habari kwa karibu zaidi kutokana na umuhimu wao.

Mchungaji Msigwa alisema CHADEMA wantarajia kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Soko Kuu la Manispaa ya Iringa, ili kuzungumza na wananchi wa manispaa hiyo masuala mbalimbali yaliyojitokeza jimboni humo.

No comments:

Post a Comment