24 September 2012
Mwandishi afukuzwa uanachama APC Arusha
Anneth Kagenda
KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC) imewataka wanahabari kote nchini, wadau na umma kwa ujumla kwamba imemfukuza uanachama Joseph Ngilisho baada ya kuridhika na malalamiko mbalimbali yaliyotolewa na yanayoendelea kutolewa dhidi yake.
Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Katibu Mkuu wa APC Bw. Eliya Mbonea ilisema, uamuzi wa kumfukuza Bw. Ngilisho umechukuliwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa APC uliofanyika Septemba 16, Mwaka huu katika Mji mdogo wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha.
Ilisema kuwa mkutano huo ulifikia maamuzi hayo baada ya kupokea na kujadili malalamiko mbalimbali dhidi ya Bw.Ngilisho yaliyofikishwa mkutanoni kutoka kwa wanachama na wadau.
"Kwa ujumla mwenendo na matendo ya mtu huyu yamevunja Katiba ya APC hasa ibara ya 9.1.19(b) na ile ya 9.1.1(f) ambapo mifano michache ikiwa ni ile ya ukosefu wa nidhamu aliyoonyesha kwa nyakati tofauti, Kufanya fujo na kutoa matusi ya nguoni mbele ya wageni katika semina ya Uandishi wa Habari na Jinsia iliyofanyika Machi 3/4/ 2011," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Ilisema baada ya kosa hilo pia alirudia akarudia kosa hilo hilo katika semina ya Uandishi wa Habari za Vijijini iliyofanyika Aprili 25/2012, Kukiuka kwa makusudi maadili ya uandishi wa habari ikiwa ni pamoja na kuandika habari za uongo na uzushi dhidi ya waandishi na wadau katika magazeti na mitandao ya kijamii.
"Pia Bw. Ngilisho anatuma meseji za vitisho, kejeli, dhihaka na matusi kwa wanachama na viongozi wa Klabu kutokana na uamuzi huo.....hivyo kuanzia tarehe ya tamko hili Klabu haimtambui tena kama mwanachama wake na wala haitajihusisha na suala lolote litakalohusiana naye," ilisema.
Taarifa ilisema wanachama hao wanauomba Umma kuelewa kwamba uamuzi huo umefikiwa baada ya hatua mbalimbali za kumuonya na kumkanya juu ya tabia zake zinazokwenda kinyume cha maadili ya uandishi wa habari kushindikana.
"Klabu inapenda kuchukua nafasi hii kutoa onyo kali kwa wanachama wake wengine wenye kukiuka maadili ya Uandishi wa Habari na kamwe hakitasita kuchukua hatua kali kwa mwanachama atakayekiuka maadili na kuitia aibu Klabu,haitakubali wanachama wake wachache wasio na maadili kuvuruga taswira njema ya sekta ya habari mbele ya wadau na umma kwa ujumla,"ilisema.
Ilisema taaluma ya uandishi wa habari ni sawa na taaluma nyinginezo ambazo zinaongozwa kwa kufuata misingi ya maadili ya kazi husika, utawala wa sheria na kuheshimiana na wala si chaka la walioshindwa maisha katika maeneo mengine.
"Pia tunapenda kuomba radhi kwa waandishi wa habari, wadau na umma kwa ujumla wake kwa yale yote yaliyotokea, na ambayo kimsingi si msimamo wa Klabu wala waandishi wenye maadili na sifa husika za kazi zao," ilisema taarifa hiyo iliyotumwa na Bw. Mbonea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment