24 September 2012
Mufti Simba alipuka Dar *Asema ang'oki ng'o, yupo tayari kwa mapambano *Aishangaa Serikali kumuacha Ponda na wenzake
Na Salim Nyomolelo
SHEKHE Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mufti Issa bin Shaaban Simba, amesema hayupo tayari kung'oka katika nafasi hiyo mbali ya shinikizo la baadhi ya wanaharakati wa Jumuiya za Kiislamu.
Alisema baraza hilo lipo tayari kwa lolote kwani lina vijana wa kutosha kwa ajili ya mapambano.
Mufti Simba aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema madaraka aliyonayo anayashikilia kwa mujibu wa katiba ya nchi hivyo jumuiya zinazompinga kama zina watu wanaojivunia, BAKWATA inao wa kutosha kabiliana nao kwa hali yoyote.
Aliongeza kuwa, jumuiya hizo zilipitishwa na BAKWATA ili kupata usajili lakini leo hii zinageuka na kuanza wapinga.
“Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zinazoongozwa na Ponda Issa Ponda, kazi yake ni kufanya ghasia, kupora misikiti, kuandamana na kudandia matukio.
“Ponda hajasoma elimu ya msingi wala dini, amekuwa akiwatumia Waislamu kwa manufaa yake na kuwachangisha fedha za kufanya maandamano ili kuwatapeli,” alisema.
Alisema kwa kuwa Ponda hajasoma elimu ya dini, hastahili kuitwa Shekhe kama anavyoitwa sasa ambapo fedha anazochangisha zimekuwa zikiishia mifukoni mwake na wenzake.
“Jumuiya hii haina hata ofisi za kuendeshea shughuli zake ambapo kikundi hiki, hakiwakilishi Waislamu wote nchini bali ni kigenge cha watu wachache wenye kufuata madhehebu ya Wamahabi.
Alisema kwa mujibu wa itikadi zao, Wamahabi wanaamini kwamba Muislamu yoyote asiyefuata itikadi yao hafai kuwa kiongozi wa ngazi yoyote.
“Vurugu na ghasia za uvamizi hazikuanzia BAKWATA, wamekuwa wakifanya hivyo katika mikoa mbalimbali, wanavamia, kuteka misikiti na kuwaondoa viongozi halali waliochaguliwa kwa nguvu na kuhodhi rasilimali za misikiti hiyo,” alisema Mufti Simba.
Alisema kikundi hicho kinatoa mafunzo ya karate katika misikiti yote waliyoiteka na kuikalia kimabavu kwa vijana wao ili waweze kuendeleza dhulma, uporaji wa misikiti na vituo vingine vya Kiislamu.
Mufti Simba alisema vitendo vya vurugu, ghasia na uvunjwaji wa sheria vinavyofanywa na Bw. Ponda, havina uhusiano wowote na dini hiyo.
Aliongeza kuwa, vitendo hivyo vinakiuka maadili ya Kiislamu na kuupa sura mbaya Uislamu miongoni mwa jamii na mataifa hivyo aliwahadharisha Waislamu na madhehebu yote kujitenga nalo.
Alisema kwa mujibu wa katiba, nchi inavitaka vyombo vya dini kuendesha shughuli zao bila ya kuingiliwa hivyo anakishangaa kikundi hicho kuingilia shughuli za BAKWATA.
“Madhehebu yote ya dini yamekuwa yakifanya shughuli zao bila kuingiliana isipokuwa kikundi hiki cha watu wachache ambacho madhehebu yao ni Wamahabi ambao wakati mwingine hujiita Answar Sunna kuingilia dhehebu lingine,” alisema Mufti Simba.
Aliwahadharisha Waislamu wote nchini kuwa Ponda si mwanazuoni wala Shekhe na hakusomea elimu ya dunia wala Quran hajui kuisoma.
Mufti Simba alitoa wito kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua wanaoleta vurugu kwa kujifanya viongozi wa taasisi hewa za dini na kutoa matamko ya kutishia kuwaondoa viongozi halali wa taasisi zilizosajiliwa na kuendesha shughuli zake kisheria.
“Naviomba vyombo vya dola vielewe si kila linalofanywa kwa kisingizio cha imani nila dini, tunaomba wasisite kuchukua hatua kwa kikundi kinachotumia anuani ya Uislamu kutenda matendo ya uvunjaji sheria,” alisema.
Hata hivyo, Mufti Simba alisema BAKWATA haipo tayari kutetea kundi lolote ambalo litajifanya Waislamu kwa kujihusisha na vitendo vinavyokiuka misingi ya dini hiyo, sheria za nchi, vurugu na kuvunja amani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment