06 September 2012
Mrema amshukia Mwenyekiti Bodi ya KNCU
Na Gladness Mboma
MBUNGE wa Vunjo, Bw.Augustino Mrema, amemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika (KNCU) mkoani Kilimanjaro, kutomtisha kwa lolote na kusisitiza kuwa hana uwezo wa kumfikisha mahakamani.
Bw.Mrema alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu.Alisema anashangaa kutolewa vitisho na Bw.Swai.
"Swai ni kama nani hadi anifikishe mahakamani? Amri ameipata wapi! Asinitishe na wala hana uwezo wa kunitisha," alisema.
Bw. Mrema alisema yeye kama mbunge hawezi kukaa kimya au kuzuiwa kuwatetea au kuhoji kitu chochote kuhusu wananchi wake bungeni, kwani tatizo la wakulima wa kahawa alilifikisha bungeni na lipo kwenye kumbukumbu za bunge.
"Sasa Swai ananitisha nini yaani anataka kunifumba mdomo, nisiwatetee wakulima wangu! Atangulie mahakamani tutaonana sitarudi nyuma, nitaendelea kuwatetea," alisema, Bw. Mrema.
Bw. Mrema alihoji uwezo wa Bw. Swai kuingilia mamlaka ya Bunge, wakati suala lenyewe lipo kwenye kumbukumbu za bunge.
Bw. Mrema alisema kuwa kamwe hatumii mbinu za kisiasa kujiweka katika mazingira magumu kwa kuwajengea chuki zisizo za msingi uongozi wa KNCU, bali alichokisema bungeni ni ukweli.
Alisema ataendelea kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu mabaki ya fedha zao, ambazo zimetokana na zao hilo na wala si vinginevyo.
Naye Mwandishi Gift Mongi, anaripoti kuwa Sakata la kutaka kufikishwa mahakamani, Bw. Mrema limezidi kuchukua sura mpya baada ya wakulima wa kahawa kutangaza maandamano hadi ofisi kuu za KNCU, ili kushinikiza kilio chao kusikilizwa.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Marangu mtoni wakulima hao walisema kuwa wameshangazwa na kitendo cha Bw. Swai, kumpinga mbunge wao badala ya kuungana naye kutetea haki.
Mmoja wa wakulima hao, Bw.Christopher Malamia, alisema Bw.Swai amewatelekeza wakulima hao na kuashiria ndiyo maana anataka kumfikisha mahakamani mbunge wao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment