Na Rose Itono
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imemwachia huru Mhasibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Justice Katiti, aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha akishirikiana na wenzake wanne na kujipatia sh.milioni 338 mali ya Benki ya Barclays Tanzania Limited.
Mshtakiwa huyo na wenzake waliachiwa kutokana na ushahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua saa nne Hakimu Mkazi, Bw. Aloyce Katemana, alisema anawaachia huru washtakiwa kwa kuwa ushahidi wa mashahidi 29 wa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Washtakiwa wengine walioachiwa huru ni Bw.Godwin Paulla, Bw.Fortunatus Muganzi, Bw.Robert Mbetwa na Bw.Gideon Otulla, wote wakazi wa Jijini Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Frederick Manyanda alisema washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 10.
Hata hivyo aliyataja baadhi ya mashtaka kuwa ni pamoja na kuitapeli benki hiyo.
Ilidaiwa kati ya Septemba 29,2008 na Oktoba 6,2008 washtakiwa wote walikula njama na kuitapeli benki hiyo.
Shtaka la pili ilidaiwa kuwa, Septemba 29 2008 washtakiwa hao kwa makusudi walighushi fomu namba E.17 ya Benki ya Barclays Tanzania Limited ya maombi ya kuhamisha fedha za mteja wakionesha kuwa Kampuni ya Tourism Promotion Services (Tanzania) Limited, iliomba benki hiyo kuilipia Kampuni ya East Africa Procurement Services Limited sh.338,935,337.46 kwa ajili ya kuiuzia mahema na vifaa vya hoteli.
Baada ya ushahidi kutolewa washtakiwa walikutwa na kesi ya kujibu na kujitetea wenyewe.
Wakati huo huo, kesi inayomkabili mfanyabiashara maarufu, Bw. Marijani Abubakari, (Papa Msofe) anayekabiliwa na shtaka la mauaji ya mfanyabiashara mwenzake, marehemu Onesphory Kitoli, imeahirishwa kutokana na kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo ilikuwa ifikishwe mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa, lakini iliahirishwa hadi Septemba 19, mwaka huu. Kesi hiyo ilikuwa itajwe Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Bi. Agnes Mchome.Upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
No comments:
Post a Comment