18 September 2012
M/kiti Halmashauri Moro atumiwa meseji za vitisho
Na Lilian Justice, Morogoro
MWENYEKITI wa Halmshauri ya Wilaya ya Morogoro, Bi. Kibena Kingo, amedai kutishiwa maisha kutokana na uamuzi wa Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kuwafukuza kazi watumishi 12 kutokana na ubadhilifu wa fedha za umma.
Bi. Kingo aliyasema hayo mjini Morogoro jana wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu mikakati aliyoweka ili kudhibiti ubadhilifu wa fedha za umma katika halmashauri hiyo.
Alisema kabla baraza hilo halijafanya kikao chake Agosti 30 mwaka huu, alitumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms), ukimhadharisha wasikae kikao hicho kwani kuna watu kutoka Shirika la Mzinga walitumwa kutega mabomu ukumbini.
“Nimekuwa nikitumiwa ujumbe wa vitisho wa mara kwa mara ili tusikae kikao lakini tuliimarisha ulinzi na kuamua kukifanya sambamba na kutoa maamuzi ya kuwafukuza watumishi hao.
“Baada ya kumaliza kikao chetu, bado ujumbe wa vitisho uliendelea kutumwa hivyo nililazimika kutoa taarifa polisi na hivi karibuni, watu zaidi ya 10, walikuja kuniulizia jirani na nyumbani kwangu bahati nzuri nilipishana nao,” alisema Bi. Kingo.
Aliongeza kuwa, kati ya watu hao mmoja alitambuliwa na ndugu zake hivyo alikwenda kuwajulisha polisi lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hali inayompa mashaka.
Alisema kutokana na hali hiyo amekuwa akifanya kazi katika mazingira magumu ya vitisho hivyo ameliomba Jeshi la Polisi mkoani humo kuchukua hatua za makusudi dhidi ya jambo hilo kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
Bi. Kingo alisema alisema kati ya watumishi walifukuzwa kazi na baraza hilo mmoja alipewa onyo kali baada ya ripoti ya tume ya Mkoa kuchunguza na kubaini ubadhilifu mkubwa wa fedha za miradi zilizofanywa na watumishi hao.
Hata hivyo, Bi. Kingo alisema mbali ya Mkoa kuunda tume, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hivi karibuni alikuwa akifanya ukaguzi hivyo idadi ya watumishi watakaofukuzwa kazi inaweza kuongezeka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Umefanya vyema sana mkuu endelea na msimamo huo. Huo ndio uongozi Bora tunaoutaka sisi na siyo maneno tu
ReplyDelete