18 September 2012

BAVICHA watakiwa kuzikabili changamoto


Na Lilian Justice, Morogoro

BARAZA la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limetakiwa kuzikabili changamoto zilizopo nchini na kuweka mikakati itakayosaidia kuchochea maendeleo ya wananchi.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw. John Heche, aliyasema hayo mjini Morogoro jana katika kikao cha vijana wa chama hicho kilicholenga kujadili masuala mbalimbali hususan hali ya siasa kwa vijana kitaifa ili kujenga Taifa moja kwa masilahi ya Watanzania.

Bw. Heche alisema nchi inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii hivyo njia mbadala inahitajika ili kuzikabili hasa kupitia vijana ambao ndio Taifa la leo na kesho.

“BAVICHA mmekuwa mkishuhudia matatizo mengi yaliyopo nchini kama mauaji, kuteswa kwa raia na wananchi kunyimwa fursa ya kushiriki mikutano ya kisiasa ambayo ni haki yao ya msingi, suala hili linapaswa kupatiwa ufumbuzi,” alisema Bw. Heche.

Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni kufa kwa viwanda ambavyo awali vilikuwa tegemeo kubwa la ajira kwa vijana nchini lakini Serikali imeshindwa kuvifufua badala yake vimetelekezwa.

“Mfano mzuri ni hapa Morogoro ambako kulikuwa na viwanda 10 ambavyo hivi sasa vimekufa hivyo vijana hawana ajira ambapo Serikali inalazimika kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi,” alisema.


Kwa upande wake, Mwanaharakati ambaye aliwawakilisha vijana wengine nchini, Bw. Jerry Murro, aliwataka vijana kuhakikisha wanapigania masilahi ya nchi kwa kupiga vita ufisadi.

“Ufisadi unarudisha nyuma maendeleo ya  nchi kwa sababu ya masilahi ya watu wachache wenye tamaa, vijana tuna fursa nzuri ya kuwa mstari wa mbele kupigania masilahi yetu na kuwafichua mafisadi wanaotumia vyeo vyao kunyonya wengine,” alisema.

Alisema asilimia 18 ya vijana wote nchini ni wasomi lakini hawana ajira hivyo ni vyema wakachukua nafasi mbalimbali za uongozi ili kuchochea maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla.

Aliwataka BAVICHA kuwa mstari wa mbele kuonesha nidhamu ili wawe mfano wa kuigwa na vyama vingine vya siasa nchini.

No comments:

Post a Comment