13 September 2012

Miss Utalii Kinondoni, Ilala kufanyika kesho



Na Amina Athumani

WAREMBO 25, wanaowania taji la Miss Utalii Ilala na Kinondoni 2012 wanatarajia kupanda jukwaa moja kesho kusaka mataji ya Miss Utalii Ilala na Kinondoni litakalofanyika katika hoteli ya Lamada, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, mratibu wa mashindano hayo Adam Bernad, alisema washindi wa mashindano hayo wa Ilala  na Kinondoni, watawakilisha wilaya zao Miss Utalii Mkoa wa Dar es Salaam.

Fainali hizi zitakuwa ni za kipekee, kwani mashabiki wa tasnia hii ya urembo watapata nafasi ya kushuhudia mchuano mkali wa warembo wa Ilala na Kinondoni," alisema Benard

Alisema mbali na warembo hao kuwania mataji ya Miss Utalii Ilala na Kinondoni, pia watapata nafasi ya kuwania mataji maalum kama Miss Utalii Vipaji, ambalo watashindana kuimba na kucheza ngoma za asili.

Mratibu huyo alisema kila mrembo atapanda jukwaani kuonesha mitindo katika vazi la ubunifu, vazi la kitalii, urembo katika vazi la kutokea na utamaduni katika vazi la asili.

Benard alisema sababu za mashindano hayo kufanyika siku moja katika jukwaa moja na ukumbi mmoja ni kuanza rasmi kwa maadhimisho ya miaka mitano ya Miss Utalii Tanzania, ambapo mwaka huu yanafikisha umri huo.

Mratibu huyo alisema zawadi za washindi ni kupata ofa masomo, katika vyuo mbalimbali nchini, kuanzia ngazi za vyeti hadi diploma.

Alisema lengo la ofa hiyo likiwa ni kuwapa zawadi za maisha washindi na washiriki, lakini pia zawadi ya elimu itanufaisha taifa, jamii na familia za warembo husika.

Mashindano hayo yamedhaminiwa Kampuni ya Business Times Limited na kituo cha Redio Times.

Wadhamini wengine ni Rashid Sports Entertainments, Tambaza Action Mart, Lamada Hotel, Pandisha Import, Oriental Bureau de Change, Eriado Point View, T Moto Entertainments na kampuni mbalimbali.

No comments:

Post a Comment