13 September 2012
Mawasiliano yaboreshwe kuleta maendeleo
Na Salim Nyomolelo
SEKTA ya mawasiliano ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo kwa kasi kutokana na utoaji wa taarifa za utendaji kazi wenye tija kwa mamlaka mbalimbali kwa muda mfupi.
Moja ya faida za mawasiliano ni pamoja kurahisisha muda jambo ambalo linasaidia utekelezaji wa majukumu kufanyika kwa wakati muafaka.
Kabla ya mawasiliano kwa njia ya simu za mkononi, watu walikuwa wakipasha habari kwa njia ya barua na simu kupitia shirika la posta na simu Tanzania ambapo ilichukua muda mrefu kupata taarifa.
Mawasiliano ya njia ya simu za mkononi yalianza kutumika nchini kuanzia mwaka 1994 jambo ambalo limesaidia kukuza na kuboresha huduma mbalimbali kwa jamii.
Ili sekta ama taasisi iweze kuendelea inahitaji kuwa na mawasiliano bora kwa muda wote ambayo itakuwa inasaidia katika kutoa fursa za kupashana habari.
TTCL ni kampuni kongwe ya mawasiliano nchini ikilinganishwa na nyingine lakini cha kushangaza huduma zake ni mbovu na zimepitwa na wakati ikilinganishwa na kampuni nyingine.
Ni kampuni ambayo ilikuwa mwenyeji wa baadhi ya kampuni za simu ambazo kwa sasa zimeshika kasi kubwa na huduma zake ni nzuri.
Uboreshwaji wa huduma katika kampuni hizo inachangiwa na kuwa na uongozi mzuri wenye tija na ubunifu wa hali ya juu kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Licha ya kupiga hatua kubwa kwa kamupuni za kigeni lakini TTCL imekuwa ikitoa huduma ambazo mimi na baadhi ya watanzania ambao ni walipa kodi hazitufai.
Miongoni mwa kampuni hizo wakati zinaanza kutoa huduma ziliazima majengo yao ambapo kwa sasa yamepiga hatua kubwa ikilinganishwa na shirika hili.
Nilivyoifahamu kampuni hii enzi hizo ni tofauti na sasa ambapo limekuwa likitoa huduma chini ya kiwango ikilinganishwa na mashirika ya kigeni kwani ilikuwa ndio mwenyeji.
Nasema inatoa huduma chini ya kiwango kwa sababu 'network' ya simu hizi inapatikana kwa baadhi ya mikoa tu na ndani ya hiyo mikoa ni baadhi ya maeneo ikilinganishwa na kampuni nyingine jambo ambalo linasababisha watu kushindwa kutumia.
Kampuni hii ni ya umma iliyokuwa ikipata ruzuku kutoka serikalini lakini cha kushangaza haina mabadiliko ya aina yoyote na badala yake uongozi unanufaika na kulipwa mishahara ambayo ni kodi zetu wananchi.
Mimi ni miongoni mwa wateja wanaotumia huduma kutoka mtandao huo lakini uzalendo unanishinda kutokana na ubovu wa huduma zake hasa unapokuwa pembezoni mwa mji.
Leo hii kama ukitokea Dar es Salaam kuelekea mikoani ukipita Kibaha tu hupati mtandao ikilinganishwa na mitandao mingine.
Nashindwa kupata jibu ni nini kinachosababisha kampuni hiyo kushindwa kuendelea na kutoa huduma zake ipasavyo ikiwa inapata ruzuku kutoka serikalini?
Serikali inatakiwa kuchunguza kwa kina kampuni hiyo ili kubaini matatizo yanayosababisha kutoendelea kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kushindwa kutoa huduma bora mikoa yote hasa kwa simu za mkononi.
Kama serikali itashindwa kuchunguza shirika hilo kwa kina itafikia mahali yatabaki majengo pekee na vyuma chakavu vya magari kwa sababu hakuna ubunifu wala jitihada za kiutendaji ambazo zinaonyesha kuwa kuna mikakati ya maendeleo.
Kuna uwezekano wa kuwepo kwa mianya ya ufisadi katika kampuni hii jambo ambalo linasababisha kushindwa kuendelea kwa miaka mingi.
Natumia nafasi hii kutoa wito kwa wahusika kuwa wabunifu lakini pia kuwa wazalendo ikiwa ni pamoja na kujiuzulu kutokana na kushindwa kuliendesha shirika hilo kwa muda mrefu.
Wakati hayo yakiendelea Wizara ya Mawasiliano nchini imebweteka, kutokana na kuonyesha jitihada za dhati hata kufanya ziara ya kushitukiza kama ambavyo anafanya Waziri wa Uchukuzi Dkt.Harrison Mwakyembe katika maeneo ya kazi zake.
Mawaziri wa wizara hii wanatakiwa kuingilia kati na kuangalia kinachoitafuna kushindwa kutoa huduma bora kwa wateja wake ikizingatiwa pia ni kampuni ya umma.
Napenda kutoa wito kwa mawaziri wa wizara hii kuwa wakati wa kupanga mikakati na uongozi wa mikakati na mchakato imepitwa na wakati na badala yake tunataka kuona utendaji na huduma bora zitolewe kwa wateja wake.
Ikumbukwe kuwa maendeleo yake ni kwa ajili ya watu wote na hivyo na tunapenda kuona linaendelea na viongozi waseme ni wapi walipokwama wasaidiwe.
snyomo@yahoo.com
0786 654410
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment