11 September 2012

Mianya ya rushwa idhibitiwe-Sumaye


Na Tumaini Maduhu

WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, amesema Serikali ina wajibu wa kudhibiti mianya  ya rushwa ambayo inawanufaisha watu wachache kwa masilahi binafsi.


Bw, Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu Huria nchini (OUT) na kusisitiza kuwa, rushwa ni adui wa haki na maendeleo hivyo  Serikali inapaswa kuweka mkakati wa kuitokomeza.

“Rushwa ni audi wa haki na maendeleo, kidogo kinachopatikana kitumike kwa maendeleo ya Watanzania wote badala ya kunufaisha watu wachache wasio waadilifu,” alisema.

Alisema Taifa lolote duniani lisipodhibiti mianya ya rushwa haliwezi kupiga hatua ya maendeleo kutokana na watu wachache kutumia rasilimali za nchi kujinufaisha.

Aliongeza kuwa, Tanzania inapaswa kutumia malighafi zake kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo zitasaidia kuleta ushindani kwenye masoko duniani.

“Tanzania tuna rasirimali nyingi kama madini ya Tanzanite, ambayo kama tutayatumia vizuri kwa kuzalisha bidhaa, tutajikomboa kwenye dimbwi la umaskini,” alisema Bw. Sumaye.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Tolly Mbwette, alisema Watanzania wanatakiwa kujiendeleza kielimu ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha.

“Watanzania tutumie fursa zilizopo kijiendeleza kielimu ili tupambane na maadui watatu ambao ujinga, maradhi na umaskini,” alisema Prof. Mbwette.

No comments:

Post a Comment