12 September 2012

Mawakala wa mizigo bandarini Dar wagoma


Na Stella Aron

MAWAKALA wa Ushuru na Forodha katika Bandari ya Dar es Salaam, jana waligoma kufanyakazi wakipinga uhakiki wa nyaraka mbalimbali kuchelewa baada ya kufanyika malipo benki hivyo kusababisha wapewa lawama na wateja wao.

Kutokana na hali hiyo, jana mawakala hao waliamua kusitisha shughuli zao na kuandamana hadi kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) Bi. Adolia Mosha, kufikisha kilio chao ili ukiritimba huo upatiwe ufumbuzi wa haraka.

Mawakala hao walidai kitendo hicho kinafanywa kwa nia ya kudhoofisha mfumo mpya wa ulipaji fedha kwa njia ya benki, ambao umeanzishwa hivi karibuni na Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe.

“Mfumo mpya wa ulipaji fedha benki hauna tatizo isipokuwa shida ipo kwenye uhakiki wa nyaraka unaofanywa na watumishi Kitengo cha Mapato, hadi muhusika apate mzigo wake ni kazi kubwa na kusababisha wateja wakose uaminifu na sisi,” walisema.

Malalamiko hayo yalimfanya, Bi. Mosha kuunda kamati ya watu watano ambayo itafanyakazi ya kuchunguza madai hayo ili yaweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Bw. Chacha Mwita, alisema kuna malalamiko ya aina hiyo, ambayo ni kero kwa wateja wao.

“Kitengo cha Mapato ndicho chenye tatizo na idadi ya watumishi waliopo ni wachache ukilinganisha na watu wanaohitaji kuhudumiwa baada ya kuwasilisha nyaraka zao,” alisema.

Bw. Chacha alisema nia ya Serikali ilikuwa nzuri ili mlundikano wa mizigo bandarini na kukwamisha juhudi za kukuza uchumi uondoke.

Juhudi za gazeti hili kumpata Bi. Mosha ili azungumzie malalamiko hayo, ziligonga mwamba kutokana urasimu uliopo kwa baadhi ya watendaji wa mamlaka hiyo.

No comments:

Post a Comment