12 September 2012

Kagasheki azungumzia maamuzi yake wizarani


Na Heri Shaaban

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema uamuzi wa kuwasimamisha kazi baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo, umelenga kupisha uchunguzi unaoendelea dhidi ya tuhuma mbalimbali za ubadhilifu zinazowakabili.


Balozi Kagasheki aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika mahojiano ya kipindi cha dakika 45, kinachorushwa na ITV.

Alisema Rais Jakaya Kikwete, alimpa nafasi hiyo ili kusimamia, kulinda rasilimali za Watanzania na kukomesha maovu ambayo yalikithiri kwa baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo.

“Nimeteuliwa na Rais kuisafisha Wizara hii, kauli ya Mbunge wa Iringa kwa tiketi ya CHADEMA, Mchungaji Peter Msigwa, kuwa watumishi niliowasimamisha ni dagaa, si kweli naomba awataje vigogo anaowajua ili tuwashughulikie.

“Aniletee orodha ya vigogo waanaohusika moka kwa moja na uhujumu katika Wizara hii ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua,” alisema.

Aliongeza kuwa, operesheni ya kukomesha maovu ndani ya Wizara hiyo kwa baadhi ya watumishi ni utekelezaji wa maagizo ya Bunge kuhusu uozo uliokuwepo na itakuwa endelevu.

“Kuhusu sakata la mauaji ya faru ni uzembe wa makusudi ambao ulifanywa na watendaji wa Wizara, hawa wanyama walipewa ulinzi mkali kama anavyolindwa Rais lakini bado wameuawa,” alisema.

Alisema gazeti la Majira ndio lilikuwa la kwanza kufichua mauaji ya wanyama hao ambapo kutokana na taarifa hiyo, Wizara ilianza kuchukua hatua za kuwasimamisha kazi baadhi ya watumishi.

Aliwataka Watanzania wampe ushirikiano katika mapambano aliyoyaanza katika Wizara hiyo ili kukomesha ufisadi uliopo na wahusika kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Akizungumzia suala la kuboresha sekta ya utalii nchini, Balozi Kagasheki alisema mwaka 2011, Wizara hiyo ilipewa dola za Marekani milioni 200, lakini hazitoshelezi ili kuvutia watalii.

Alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa za majangili ambao wanaihujumu sekta hiyo waweze kukamatwa.

No comments:

Post a Comment