13 September 2012

Mashindano ya ngumi yasogezwa


Na Amina Athumani

SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa  Tanzania (BFT), limeyapiga kalenda mashindano ya Taifa hadi Septemba 17 mwaka huu yatakayofanyika katika Uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam.


Awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika Septemba 15, mwaka huu lakini yameahirishwa kutokana na uwanja huo kuwa na shughuli nyingine.

Uwanja huo kwa sasa unatumiwa na Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD) kwa ajili ya mashindano yake ya mkoa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema lengo la mashindano hayo ni kupata timu ya taifa ya ngumi yenye sura ya kitaifa.

"Mashindano yatashirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara tumeanza maandalizi ya mapema na ya uhakika kwa ajili ya kupata wachezaji bora watakaoshiriki mashindano mbalimbali.

"Mashindano yanayotukabili ambayo tumepania kufanya vyema ni Jumuiya ya Madola 2014, Afrika 2015, Olimpiki 2016, ubingwa wa Dunia na mengine tutakayopewa mialiko," alisema Mashaga.

Alisema hadi jana mikoa 18 imeshathibitisha kushiriki mashindano hayo.

Mashaga alisema mashindano yatagharimu sh. milioni 26 kwa ajili ya malazi, maandalizi na chakula kwa mabondia watakaoshiriki.

No comments:

Post a Comment