13 September 2012

Kocha Azam amtupia lawama mwamuzi



Na Zahoro Mlanzi

BAADA ya kushuhudia timu yake ikichapwa mabao 3-2 na mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba Kocha wa Azam FC, Bunjak Boris ameshangazwa na maamuzi yaliyotolewa na mwamuzi, Martine Saanya aliyechezesha pambano hilo.

Kauli hiyo aliitoa, mara baada ya kumalizika mechu hiyo iliyopigwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushuhudiwa na maelfu ya mashabiki wa soka nchini.

Boris alisema walicheza vizuri katika mechi hiyo, lakini  mwamuzi hakuitendea haki timu yake kwani imenyimwa penalti mbili za wazi na kuipa Simba penalti isiyo halali, wakati tukio hilo likitokea yeye (mwamuzi) alikuwa nyuma ya wachezaji na aliyepaswa kuamua hivyo ni mwamuzi msaidizi.

"Sijui labda ndivyo soka la Tanzania lilivyo, lakini tangu nianze kulijua sijaona maamuzi kama haya na isitoshe mimi waamuzi wa Tanzania siwajui inawezekana kukawa na sheria nyingine," alilalamika Boris.

Alisema pamoja na mambo hayo wamepoteza nafasi nyingi za kufunga na inavyoonekana wachezaji wake walishindwa kuumudu mchezo, kadri muda ulivyokuwenda kutokana na maamuzi ya mwamuzi huyo.

Kocha huyo alisema anapenda kuwa na timu iliyokamilika ikiwa na wachezaji 11 na si kusubiri wachezaji wa akiba kuleta mabadiliko, ila inapobidi huamua kufanya hivyo kulingana na mechi husika.

Alisema kwa sasa kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya ligi hiyo, ambapo leo au kesho itakwenda Bukoba kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Kagera Sugar, itakayopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini humo.

Akizungumzia kuhusu ligi hiyo kwa ujumla, Boris alisema watahakikisha wanapigana kufa au kupona kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mwaka huu, kwani kikosi alichonacho kina wachezaji wazuri.

No comments:

Post a Comment