18 September 2012

Madiwani Moshi wamshukia RC


Na Gift Mongi, Moshi

MADIWANI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamedai kitendo cha Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Leonidas Gama, kuzuia safari yao ya kwenda Kigali nchini Rwanda, kimewasikitisha.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya madiwani hao wamemtaka Bw. Gama kuacha kufanya shughuli za kisiasa badala yake awajibike kutekeleza sera za kuchochea maendeleo ya wananchi.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa madiwani hao Bi. Hawa Mushi, alisema kitendo alichokifanya Bw. Gama ni kuwakandamiza madiwani wa manispaa hiyo kwani mapato ya ndani yameongezeka hivyo hakukuwa na sababu ya kuwazuia.

“Safari yetu inetumia sh. milioni 123 tu, tulikubaliana tupewe posho za siku tatu na ile ya nne tusipewe lakini Bw. Gama alipinga tusiende akidai bajeti iliyotengwa ni kubwa,” alisema.

Bw. Gama alipinga safari hiyo kwenye Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa ambacho kilihudhuriwa na madiwani pamoja na baadhi ya wakuu wa Idara Manispaa ya Moshi.

Alisema safari hiyo haina tija kama inatumia kiasi kikubwa cha fedha ambapo agenda waliyokuwa wakienda kuizungumza ni utunzani mazingira katika mji huo.

No comments:

Post a Comment