18 September 2012
'Halmashauri Dar zitenge maeneo ya Bodaboda'
Na Darlin Said
HALMASHAURI za Mkoa wa Dar es Salaam, zimeshauriwa kutenga maeneo ambayo yatatumika kupaki pikipiki zinazofanya biashara ya kubeba abiria maarufu (bodaboda).
Kaimu Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Jordan Lugimbana, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizindua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.
Kauli mbiu ya wiki hiyo mwaka huu inasema, “Pambana na ajali za barabarani kwa vitendo, zingatia sheria”.
Bw. Lugimbana alisema kuzagaa kwa bodaboda katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo, kunachangiwa na wafanyabiashara hao kukosa maeneo ya kupaki hivyo kutengwa kwa maeneo hayo, kutasaidia kuondoa tatizo lililopo sasa.
“Natoa wito kwa Kamati ya Usalama Barabarani kuhakikisha hizi bodaboda zinasajiliwa ili zitambukilike kama mnavyofanya kwenye teksi ili muweze kuzitambua kila Wilaya,” alisema.
Ili kuhakikisha tatizo la ajali za pikipiki zinapungua, Bw. Lugimbana aliliomba Jeshi la Polisi kuwasimamia watu wote waliopewa jukumu la kusimamia sheria za usalama barabarani.
“Polisi mnapaswa kuwa makini na usimamizi wa sheria kwani waendesha bodaboda ndio wanaongoza kwa kupata ajali,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani mkoani humo, Bw. Elifadhili Mgonja, alisema Mkoa huo unaongoza kwa ajali ukilinganisha na mikoa mingine nchini.
“Mwaka huu ajali zimeongezeka ukilinganisha na 2010/11, hali hii imetokana na ongezeko la bodaboda hivyo lazima tutoe elimu kwa
watumia barabara,” alisema.
Bw. Mgonja alisema kamati yake imejipanga vizuri kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa ili kumaliza tatizo la ajali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment