19 September 2012

Madaktari wageukana *Jumuiya yadai utetezi wao ni dhaifu sana



Na Salim Nyomolelo

JUMUIYA ya Madaktari nchini, imesema msahama ulioombwa na madaktari waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo ambao Serikali iliwafutia vibali vya kazi ni dhaifu kwa sababu walishiriki mgomo huo kwa hiari yao bila kushinikizwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dkt. Godbless Charles, aliitaka Serikali kuzingatia sheria ili kuamua kama madaktari hao wanastahili msamaha wa kurudi kazini.

Alisema madaktari hao hawakulazimishwa kugoma badala yake walishiriki mgomo huo kwa hiari yao lakini baadhi yao walikuwa wakiendelea na kazi.

“Hatujui kwa nini waombe radhi kwa Rais Kikwete na Watanzania, wamefanya kosa gani, wao walikuwa wakifanya kazi chini ya   uangalizi wa Madaktari Bingwa ambao ndio waligoma hivyo wasingeweza kushtakiwa.

“Hawa madaktari wanafunzi wasingeweza kuendelea kutoa huduma kwa sababu Madaktari Bingwa waligoma hivyo wakuulizwa si wao, madaktari hawa walishiriki migomo yote mitatu na miongoni mwao, walikuwa wakiendelea na kazi sasa kwanini waseme waligoma kwa kushawishiwa,” alisema Dkt. Charles.

Alisema kuwa, madai ya madaktari hao ni mchakato ambao utaendelea kwa vizazi vya sasa na vijavyo licha ya kujitokeza kikundi au mtu kuwatumia ili waombe msamaha ili kuidhalilisha taaluma hiyo pamoja na kurudisha nyuma jitihada za kuboresha huduma za afya nchini na masilahi ya watumishi.

Aliongeza kuwa, vikao mbalimbali walivyokaa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi na maofisa wengine wa Wizara hiyo, walisisitiza kuwa suala hilo lipo kisheria hivyo wameshangazwa na kitendo cha wenzao kuomba radhi.

“Tunaliomba Balaza la Madaktari Nchini (MCT), litekeleze majukumu yake ili kuharakisha upatikanaji wa haki,” alisema.

Alisema kamati ya jumuiya hiyo imejiandaa kuhakikisha inaweka wakili pale ambapo madaktari hao wataanza kuhojiwa kwani sheria ya MCT inatoa fursa hiyo.

Akijibu maswali ya waandisi wa habari, Katibu wa jumuiya hiyo, Bw. Edwin Chitale, alisema uwezo wa kuhimili maisha miongoni mwa madaktari unatofautiana hivyo kila mtu yupo huru kufanya uamuzi wake.

“Wote walioridhia kuomba msamaha inawezekana wameshinikizwa kufanya hivyo, hadi sasa hakuna hata dai moja ambalo Serikali imelitekeleza ili kuboresha huduma za matibabu,” alisema.

Akizungumzia suala la kupandishiwa mishahara Bw. Chitale, alisema ni utaratibu wa kawaida kwa Serikali kufanya hivyo kila mwaka wanaposoma bajeti.

Alisema wao hawawakani madaktari hao bali dhamira ya mgomo si kuomba msamaha bali kwa ajili ya kudai masilahi ya msingi ambayo hadi sasa Serikali imeshindwa kuyatekeleza.

Hata hivyo, jumuiya hiyo imetoa wito kwa madaktari hao kutumia hekima na busara katika kipindi hiki kigumu ili kuepuka kutumiwa na kikundi cha watu wenye masilahi binafsi.

Wakati huo huo, Mwandishi wetu Goodluck Hongo, anaripoti kuwa,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, jana ilishindwa kutoa msimamo wao kama msamaha huo wameupokea.

Mwandishi wetu alifika wizarani hapo ili kupata msimamo wa Wizara ambapo Msaidizi wa Ofisa habari Bi. Catherine Sungura, alisema Ofisi ya Msajili wa Madaktari ndio wanaoweza kulizungumzia suala hilo.

“Nawaomba muende Ofisi ya Msaliji wa Madaktari ndio wahusika wakuu, bosi wangu hayupo (Bw. Mwamwaja), hivyo nendeni huko mtapata majibu ya maswali yenu,” alisema.

Baada ya mwandishi kufika katika ofisi hiyo, aliambiwa aende kwa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Donan Mmbando ambaye naye aliwarudisha kwa Bi. Sungura ambaye alilisukuma suala hilo kwa Ofisa Habari Mkuu wa Wizara hiyo ambaye hakuwepo.

No comments:

Post a Comment