10 September 2012

Lissu, Nape watoana jasho


Na Reuben Kagaruki

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye na Mkurugenzi Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Tundu Lissu, jana walitoana jasho katika kipindi cha 'Tuongee Asubuhi' ambacho kinarushwa na Kituo cha Star Televisheni.

Katika kipindi hicho, vigogo hao kutoka vyama vyenye upinzani mkali, kila mmoja alikuwa akijenga hoja za kujinasua na hoja ya kuhusika na mauaji yenye sura za kiasia. 

Katika kipindi hicho kilichorushwa asubuhi, Bw. Lissu alikumbushia matukio ya mauaji yaliyotokea katika maeneo mbalimbali nchini kwenye shughuli za kisiasa na kulituhumu Jeshi la Polisi.

Alitolea mfano wa mauaji ya watu watatu yaliyokea jijini Arusha, katika maandamano ya CHADEMA na kada wa chama hicho ambaye aliuawa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo mjini Igunga, mkoani Tabora, Oktoba 2011.

Mauaji mengine ni yale yaliyotokea Kata ya Ndago, mkoani Singida muda mfupi baada ya kumalizika mkutano wa chama hicho, yaliyotokea mkoani Morogoro na Iringa yakihusisha kifo cha mwandishi wa habari, marehemu Daudi Mwangosi.

Alisema polisi ndio wahusika wa mauaji hayo na kusisitiza kuwa, CHADEMA inaongoza kwa mikutano na shughuli nyingine za kisiasa. 

Baada ya maelezo hayo, Bw. Nape alipewa nafasi na alionesha kukerwa na kauli ya Bw. Lissu, akimtaka aache kusema uongo.

“Katika mauaji ya Singida, aliyeuawa ni kada wa CCM baada ya mkutano wa CHADEMA kumalizika, kada wetu mwingine alimwagiwa tindikali katika uchaguzi wa Igunga.

“Ni jambo la kushangaza kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, (Dkt. Willibrod Slaa), kuongoza operesheni zinazosababisha mauaji bila kujiuliza kwanini haya yanatokea...hili ni jambo la kushangaza,” alisema Bw. Nape.

Alisema si kweli kwamba CHADEMA kinafanya mikutano mingi ya kisiasa nchini kuliko chama kingine chochote.

“Haiwezekani viongozi wote wa chama hiki wafunge ofisi na kwenda kufanya mikutano, huu ni umaskini,” alisema, Bw. Nape.

Bw. Lissu alipewa nafasi nyingine na kusema kuwa, kwanza anashukuru CCM inakubali chama chao ni maskini maana mara nyingi amekuwa akisema CHADEMA inapata fedha kutoka nje.

Baada ya kusema hayo, Bw. Nnauye aliingilia kati majibu hayo na kusema kuwa; “Sikusema umaskini wa fedha, bali wa mawazo”.

No comments:

Post a Comment