19 September 2012

Jeta aipangia mikakati Simba Shibam


Na Mwali Ibrahim

SIKU chache baada ya kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Tawi la Simba Shibam Magomeni, Dar es  Salaam, Ismail Jeta ameanika mikakati yake atakayoanzanayo.

Jeta alichaguliwa hivi karibuni katika uchaguzi mdogo uliofanyika baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa tawi hilo, Soud Ramadhani kulazimishwa kujiuzulu kutokana na mgongano wa maslahi aliokuwa nao na Klabu ya Villa Squad kwa kuwa kiongozi wa timu hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana Jeta, alisema ni aibu kwa tawi kongwe kama hilo, ambalo limekuwa kinara kwa kutoa Wenyeviti wa Simba wenye uzoefu wa soka, kuwa halina ofisi huku likishindwa kujiendesha kutokana na mikakati dhaifu ya kiuchumi iliyokuwapo.

"Hassan Dalali ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Simba ni mmoja ya wanachama wa tawi hilo, Said Pamba na Ismail Aden Rage Mwenyekiti wa sasa wa klabu hiyo, akiwa miongoni mwao.

"wanachama sasa tunatakiwa kuwa na ofisi yetu ambapo tutakuwa tukikutana kupanga mikakti mbalimbali," alisema.

Aliongeza kuwa wanajipanga kuhakikisha tawi hilo linakuwa kiuchumi na kuleta tija pamoja na kuwa mchango mkubwa kwa klabu hiyo.

Alisema ili kufanikisha mikakati ya kimaendeleo aliyonayo ni vyema wanachama wakasahu tofauti  zilizokuwapo wakati wa uchaguzi na wakaungana ili kujenga misingi imara itakayoisadia Simba kutetea taji lake la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Viongozi wengine katika tawi hilo ni Katibu Athumani Ally, Makamu Mwenyekiti Juma Dadi, Mhazini Said Ndembo, mlezi Diwani wa Kata ya Magomeni Julian Bujugo, huku Chano Almas, Ramesh Patel na Filipo Kitambia wakiwa wadhamini.

No comments:

Post a Comment