24 September 2012

JK alishauri Bunge EAC



Na Jesca Kileo

RAIS Jakaya Kikwete, amelishauri Bunge la Afrika Mashariki, kuzingatia na kufuata maelekezo yaliyomo katika mkataba ulioanzisha jumuiya hiyo wanapowakilisha na kujadili hoja zao.

Alisema jumuiya hiyo inahusika na masuala yaliyomo katika mkataba na itifaki ambazo ndio zimeanzisha jumuiya na kila nchi ina wajibu wa kuzingatia kilichomo kwenye mkataba.

Rais Kikwete aliyasema hayo Ikulu, Dar es Salaam juzi alipokutana na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Bi. Margareth Ziwa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jana, ilisema Rais Kikwete alilitaka Bunge hilo lisisahau kuwa nchi zote wanachama zina sheria na taratibu ambazo wanapaswa kuzifuata na kuzizingatia.

“Bunge hili linaweza kutoa ushauri lakini si kuzielekeza au kuzilazimisha nchi wanachama kutekeleza jambo ambalo halimo kwenye mkataba ambao zimetiliana saini,” alisema.

Bi. Ziwa ambaye ni raia wa Uganda, alifika Ikulu kujitambulisha kwa Rais Kikwete baada ya kushika wadhifa huo hivi karibuni.

Rais Kikwete aliwataka wabunge wapya kusoma mkataba na itifaki zilizoanzisha jumuiya hiyo ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri bila kuingilia uhuru na taratibu za nchi wanachama.

No comments:

Post a Comment