25 September 2012

Kikwete awashukia wapinzani wa CCM *Adai wanaokiombea kife watakufa wao *Hatima ya wagombea kujulikana kesho



Na Pendo Mtibuche, Dodoma

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Jakaya Kikwete, amesema kamwe chama hicho hakitakufa na wanaokiombea kife, watakufa wao na kukiacha kikiwa hai.


Rais Kikwete aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akifungua Kikao cha Kamati Kuu (CC) na kuongeza kuwa kikao cha Kamati ya Maadili kilichomalizika jana saa tisa usiku, kilikuwa na jukumu la kupitia majina mengi ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

“Dhamira yetu ni kutenda haki kwa wagombea wote walioomba nafasi husika ambao walikuwa wanafikia 5,000, hivyo wajumbe wa Kamati ya Maadili wametumia muda mwingi kuyachambua,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa, kikao hicho kimeweza kufanya mabadiliko tofauti na yale yaliyotoka mikoani kwa kupitia majina ya waliopitishwa kugombea Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kutoka mikoani wengi wao wakiwa wasomi.

“Tumejaribu kujihoji wenyewe kwanini huyu kapewa alama hii na yule kanyimwa ndio maana nasema kasi haikuwa ndogo kupitia jina moja moja na kutoa mapendekezo,” alisema.

Rais Kikwete alisema madadiliko ya utoaji alama kwa wagombea yatarahisisha uteuzi wa majina katika kikao cha NEC ambacho kinatarajiwa kufanyika kesho.

“Kikao cha kamati ya maadili kilikuwa kikubwa zaidi kilichohitaji umakini mkubwa, lengo ni kupitia majina kwa usahihi lakini kikao cha NEC natarajia kitakuwa chepesi na kitaisha mapema,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, kikao cha NEC kitakuwa na kujumu la kupitisha majina ya wagombea wanaofaa.


1 comment:

  1. Historia inatujuvya kwamba hakuna kiongozi aliyewahi kukubali kwamba chama chake kinakufa. Aidha ni hulka ya binadamu kupingana na ukweli hasa ukweli unapotishia mapenzi yake kwa kitu au mtu akipendacho. Kwa wanasiasa, si mapenzi tu unaowasukuma kupingana na ukweli bali hofu ya kukosa madaraka, heshima na maslahi yanayoambatana na madaraka hayo. Tuliona kule Kenya, Romania, Malawi, Uganda, Zambia, Libya, Iraq, na kwingineko. Leo vyama hivyo ni vya upinzani, vingine vimepigwa marufuku, vingine hata kuvaa sare zake ni aibu, vingine vimejifia, n.k. CCM endeleeni na kupingana na ukweli mtaona matokeo yake. Chama kikishakalia mgongo wa polisi, jeshi na usalama wa taifa ni dalili tosha kimeshakufa! Mkakati sasa ungekuwa kuandaa mazingira ya kuteremka kutoka mbeleko ya dola iliyowabeba. Ukiona mtoto amekuwa kijana na hatimaye mtu mzima lakini bado anabebwa na mbeleko na kunyonya dole gumbe ujue hakuna mtoto hapo!

    ReplyDelete