14 September 2012
Kikapu wamleta kocha Mmarekani
Na Amina Athumani
SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani, Serikali ya Tanzania, wamemleta kocha raia wa Marekani kwa ajili ya kufundisha timu ya Taifa ya mchezo huo kwa kipindi cha miaka minne.
Kocha huyo ni Albert Sokaitis atakayekuwa kocha mkuu akiambata na Msaidizi wake, Jocquis Sconiers ambao wote wataifundisha timu ya Tanzania ya mpira wa kikapu ya wanawake na wanaume katika kipindi cha miaka minne.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa (TBF), Phares Magesa alisema makocha wote watawasili nchini Septemba 21, mwaka huu na wataanza kazi rasmi Septemba 22, mwaka huu.
Alisema Sokaitis ambaye atakuwa kocha mkuu wa timu hiyo ana uzoefu wa kipindi cha miaka 24 katika mchezo huo ambapo mpaka anakuja nchini alikuwa ni Kocha Mkuu wa timu ya Chuo kikuu cha Post cha nchini Marekani kilichopo jimbo la Connecticut.
Alisema kocha huyo pia amewahi kufundisha timu na kuendesha mafunzo katika nchi za China, Lebanon, Ugiriki na Japan.
"Makocha hawa watafundisha timu zetu zote za taifa na pia kufundisha makocha wetu wazalendo na pia kocha huyu mkuu ndio atakuwa mshauri mkuu wa kiufundi kwa TBF,"alisema Magesa.
Alisema makocha wote wana shahada za juu kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Marekani na na kwamba TBF imewateuwa makocha wasaidizi wazalendo wanne watakoofanya kazi na walimu hao wa kigeni.
Aliwaja makocha wazalendo ni Everist Mapunda (kutoka Klabu ya Pazi), Leonard Kwale (kutoka Klabu ya ABC), Agnella Semwaiko (kutoka Klabu ya Don Bosco Lioness) na Bahati Mgunda (kutoka Klabu ya Vijana) ambao watatangaza vikosi vya timu za taifa za wanawake na wanaume mapema wiki ijayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment