12 September 2012

Askari JWTZ wadaiwa kushambulia wananchi


Na Bryceson Mathias, Kilindi

MWENYEKITI wa Kitongoji cha Kwasamuge, Kijiji cha Bunila, Kata ya Kinde, Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, Bw. Juma Swai, amelalamikia kitendo cha baadhi ya askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuwashambulia wananchi kwa kuwapiga bila sabbu za msingi.

Inaelezwa kuwa, chanzo cha wanajeshi hao kutoa kipigo kwa wananchi ni baada ya kuvamia kijijini hapo na kutaka kunywa pombe za kienyeji bure bila kutoa malipo yoyote.

Akizungumza na gazeti hili jana Bw. Swai alisema wanajeshi waliotoa kipigo hicho kwa wananchi ni wakufunzi wa mafunzo ya mgambo katika Kambi ya Nyadigwa, Kata ya Kinde.

Alisema tukio hilo limetokea hivi karibuni ambapo wanajeshi hao walikuwa wanne ambao walifika kijijini hapo wakiwa kiraia na baada ya kuulizwa vitambulisho vyao, walianza vitisho na kutaka kunywa pombe za kienyeji bure.

“Kila nilipotaka watoe vitambulisho ili niwatambue haawkuwa tayari kutoa ushirikiano na baada ya kuwatilia mashaka kuwa ni wezi, waliondoka na kurudi kesho yake wakiwa na sare za jeshi.

“Walipofika hapa kijijini, walianza kuwashabulia wananchi kwa kuwapiga ambapo hivi sasa kuna uadui mkubwa, zipo taarifa zinazodai na mimi natafutwa ili wanidhuru,” alisema.

Bw. Swai aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo alilazimika kutoa taarifa za uhasaba huo kwa Mtendaji Kata, Bw. Muharami Sudi na Diwani wa Kata ya Kilindi, Bw. Shabani Bonge.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Selemano Liwova, alikiri kupokea taarifa hizo toka kwa Bw. Bonge na kusema tayari tatizo hilo amelifanyia kazi.

“Nimemwagiza Katibu Tarafa aende kwenye kambi hiyo ili aweze kupewa taarifa ambayo ndio itafanyiwa kazi na mimi nitawasiliana na Mshauri wa Mgambo ili tuangalie njia ya kulimaliza,” alisema.

Kwa upande wake, mbunge wa jimbo hilo, Bi. Beatrice Shelukindo, alipopigiwa simu ili kujua kama ana taarifa zozote juu ya tukio hilo alisema yupo kwenye kikao mkoani Tanga na kuahidi kulifuatilia.

“Kuna matukio karibu matano yamejitokeza katika eneo hilo likiwemo la umavizi wa maeneo kwa watu kutoka nje ya eneo husika, hivyo ni kweli wameanza kuishi kwa hofu katika maeneo,” alisema Bi. Shelukindo.

No comments:

Post a Comment