24 September 2012

JK awatolea 'uvivu' wanasiasa *Dkt. Dau aombewa nishani ya utumishi bora


David John na Andrew Ignas

RAIS Jakaya Kikwete amewaonya watu wanaotunga uongo kama sehemu ya utamaduni wao na kumuandika katika mitandao kuwa ameliuza eneo la Kigamboni kwa Rais mstaafu wa Marekani Bw. George Bush.

Alisema thamani kubwa ya vyama vya siasa ni maendeleo ya wananchi lakini baadhi ya vyama hivyo havifurahii maendeleo yanayoletwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Kigamboni, ambayo ilifanyika eneo la Kurasani.

“Baadhi ya wanasiasa na vyama vyao wahapendi daraja hili lijengwe na leo hawatalala usingizi, kazi ya vyama vya siasa ni kuweka masilahi yetu sote mbele.

“Watu wana viwanda vya kuzalisha uongo katika mitandao na maeneo mengine, wamewahi kusema mimi nimemuuzia Rais mstafu wa Marekani Bw. George Bush eneo la Kigamboni, huu ni uongo mkubwa Bush aje kufanya nini Kigamboni,” alihoji Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa, wapo baadhi ya watu ambao hawapendi maendeleo yanayoletwa na Serikali kwa wananchi wake lakini watakufa kwa kihoro kwa sababu hawatashindwa bali kila waliloahidi watalifanya na kufanikiwa.

Alionya kuwa, Serikali yake haitaruhusu mtu yoyote kuzuia au kuchelewesha miradi ya maendeleo inayolenga kunufaisha watu wengi ambapo ujenzi wa daraja hilo utapunguza adha ya usafiri.

“Hivi sasa tunategemea vivuko, boti ndogo na mitumbwi ambapo wenye magari kulazimika kufanya mzungumo wa kilomita 52.

“Kwa uamuzi wa sasa, watembea kwa miguu watakuwa na sehemu maalumu katika daraja hili na waendesha baiskeli watavuka bure bila malipo yoyote,” alisema.

Rais Kikwete aliongeza kuwa, Serikali haiwezi kudhulumu wananchi wake hivyo wote ambao wanastahili kulipwa fidia kutokana na ujenzi wa daraja hilo na Mji Mpya wa Kigamboni watalipwa stahiki zao.

Daraja hilo ambalo wazo la ujenzi wake lilibuniwa mwaka 1978, zaidi ya miaka 30, wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, litagharimu sh. bilioni 214.6.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, daraja hilo litakamilika baada ya miezi 36, ingawa muda huo unaweza kupungua na kubakia 30.

Alisema daraja hilo litakuwa na urefu wa mita 680 ambapo gharama za ujenzi wake zinafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 40 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) asilimia 60.

Wakati huo huo, Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli, amemuomba Rais Kikwete, kumpa Nishani ya Utendaji Kazi Uliotukuka Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dkt. Ramadhan Dau.

Akizungumza kabla Rais Kikwete hajaweza jiwe la msingi, Dkt. Magufuli alisema Dkt. Dau unastahili kupata nishani hiyo kutokana na jitihada zake za kuendeleza miundombinu ya Taifa.

Alisema wakati umefika kwa Watanzania kutambua mchango wa viongozi wazalendo, kama ilivyo kwa Dkt. Dau, ambaye amesaidia kkufanikisha ujenzi wa daraja hilo.

“Mheshimiwa Rais, tumezoea kukuona ukitoa nishani kwa wanajeshi kutokana na utendaji kazi wao, lakini wapo wananchi wengine kama Dkt. Dau wanaostahili kupata nishani kutokana na utendaji kazi wao kwa Taifa,” alisema, Dkt. Magufuli.

Aliongeza kuwa, Dkt. Dau na wenzake wanastahili kupata nishani za utendaji kazi uliotukuka kutokana na jitihada kubwa za kubuni na kusimamia miradi ya maendeleo yenye tija kwa nchi.

Alisema ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Daraja la Kigamboni, Machinga Comlex na nyumba za bei nafuu zilizojenga katika mikoa mbalimbali nchini ni kielelezo kuwa Dkt. Dau ni mchapakazi anayestahili kupewa nishani ya Rais.


No comments:

Post a Comment