19 September 2012

Ukata wakumba mashindano ya ngumi


Na Mwali brahim

SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), limelazimika kurudisha nyuma tarehe ya kumaliza mashindano ya Taifa baada ya kukumbwa na ukata wa fedha.

Mashindano hayo ambayo yanaendelea katika Uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam awali yalipangwa kumalizika Jumamosi, lakini kutokana na wamelazimika kuyamaliza kesho. Mashindano hayo yanashirikisha mabondia 109 kutoka mikoa 18.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema mashindano hayo yanafanyika kwa hali ngumu kutokana na kukosa wadhamini, ambapo awali waliomba udhamini katika kampuni na wadau wa michezo 30 lakini hakuna aliyeweza kujitolea.

Alisema tatizo kubwa linalowakabili ni chakula kwa wachezaji na vifaa vya michezo, huku mwaka huu timu nyingi zimeshiriki.

"Mashindano hayo tunayafanya katika hali ngumu mno, lakini kwa kuwa yapo katika kalenda yetu tumelazimika kufanya na tunaipongeza mikoa kujitokeza kwa wingi, lakini pia tunaiomba serikali kutusaidia kupata udhamini wa kudumu hata kwa baadaye," alisema.

Naye Mjumbe wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), ambaye alifungua mashindano hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wa baraza hilo Deoniz Malinzi alisema wao kama serikali wametoa sh. milioni 2, ili BFT ifidie upungufu uliokuwepo.

"Nadhani fedha hizi zitasaidia japo kidogo kufidia upungufu uliokuwepo katika mashindano haya, lakini pia tunawataka na nyinyi mtafute wadhamini isi tutawasaidia pale mtakapopungukiwa," alisema.

Aliongeza kuwa, anawapongeza wachezaji wote wasaliojitokeza, makocha, waamuzi na madaktari na kuwataka kujituma kwa ili kurudisha imani ya mchezo huo kama awali.

Katika mapambano ya uzito wa kg. 56 yaliyochezwa jana bondia Emillian Patrick (JKT) amemtwanga Thomas Soni (Temeke) kwa KO baada ya mwamuzi kumwokoa, Undule Langson (Magereza) akimchapa Hashim Leonard (Mtwara) kwa kuokolewa na Hussein Mrumbo (Kilimanjaro) aliyeshinda pia kwa KO dhidi ya Bakari Msame (Mbeya).

Bashiri Mrisho (Arusha) alidundwa na Omari Mrisho (Dodoma) kwa pointi 4-1 huku Elirayige John (Kilimanjaro) alimchapa Mawazo Samweli (Polisi) kwa pointi 3-1 na Leeroy John (Manyara) na Palygod Kinyaa (Mororgoro) walipewa ushindi baada ya wapinzani wao kuingia mitini.

No comments:

Post a Comment