19 September 2012

I-View kurekodi video mpya ya Diamond


Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI I-View Studios ya Dar es Salaam imeshinda mchakato wa kurekodi video mpya ya msanii Naseeb Abdul ‘Diamond’ ambayo usaili wake utafanyika Jumamosi Nyumbani Lounge.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya One Touch Solutions, Petter Mwendapole alisema I-View imepata nafasi hiyo kutokana na kiwango kikubwa cha video kadhaa ilizofanya, lakini pia vifaa ilivyonavyo.

“Siku zote kila mtu anaangalia kitu kizuri, Diamond ametaka kufanya mapinduzi katika tasnia ya muziki, lakini kufanya mapinduzi kunahusisha vitu vingi, tungo zake yeye kama msanii, studio anayorekodia watu, lakini mwisho wa siku I-View chini ya Raqey Mohamed ndiyo imeshinda nafasi hiyo.

Kwa upande wake Raqey ambaye ni Mkurugenzi wa I-View, alisema anahitaji kuifanya kazi hiyo kuwa tofauti ili kusukuma mbele sekta ya mawasiliano na muziki kwa ujumla.

“Sisi kama I-View tunafurahi kufanya kazi na Diamond ni msanii mzuri na mkubwa ambaye kazi zake zinaonekana, hatutamuangusha, mashabiki na wasanii wengine wasubiri kazi itakapotoka,” alisema.

I-View pia itashiriki katika mchakato wa kupata watu watakaonekana kwenye video hiyo, ambayo ni kwa mara ya kwanza nchini kufanyiwa usaili wa washiriki.

Usaili huo utafanyika Jumamosi Nyumbani Lounge. Majina ya majaji watakaochuja yatatangazwa leo.

No comments:

Post a Comment