19 September 2012

ADC yajipanga kuinua vipaji Temeke


Na Anneth Kagenda

CHAMA kipya cha siasa cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilaya ya Temeke, kimejipanga kuhakikisha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana ili kuwaondoa katika janga la kutumia dawa za kulevya.


Akizungumza Dar es Salaam mwishoni mwa wiki Mwenyekiti wa ADC Wilaya hiyo, Salum Soud alisema lengo si tu kujinadi kwa propaganda, bali kuwakomboa wananchi wake na umaskini pamoja na vijana.

Soud alisema kutokana na kwamba vijana ndiyo wachapakazi katika taifa, wanatakiwa kuwezeshwa kwenye mambo mbalimbali, lakini kubwa ni michezo ili waondokane na mambo hayo pamoja na vyama vingine kuwatumia katika maandamano yasiyo na tija kwao.

"Tunatarajia kuanzisha ligi za michezo mbalimbali ikiwemo soka, kikapu na riadha kwa vijana wa wilaya yetu ili kuwanusuru katika makundi ambayo hayawaletei maendeleo yoyote yakiwemo maandamano yasiyo ya lazima," alisema.

Alisema hivi sasa ADC, iko kwenye mchakato wa kuhamasisha vijana wa wilaya hiyo, ili wapate mwamko wa kujiunga na michezo na badaye watatoa ratiba baada ya kuwasiliana na Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Temeke (TEFA).

Mwenyekiti huyo alisema mashindano hayo pia yatashirikisha wanawake, ambao wametakiwa kujitokeza kushiriki na kuwa watazamaji.

No comments:

Post a Comment