06 September 2012
Elimu utunzaji misitu utapunguza ukataji miti
Na Rose Itono
PAMOJA na serikali kuwa mstari wa mbele kuhakikisha inalinda maliasili ya nchi kwa kuzuia uharibifu wa misitu kwa kuvuna miti hovyo bado hali hiyo itakuwa ngumu kuwawajibisha viongozi wanaowaachia wahalifu.
Kukithiri kwa uharibifu wa mazingira nchini kunatokana na viongozi kuanzia ngazi ya mtaa kubweteka bila kuwajibika na kuwafichua waharibifu wa misitu.
Sekta ya Misitu katika nchi zinazoendelea inakadiriwa kuchangia uzalishaji wa hewa ukaa hadi kiasi cha asilimia 18 kutokana na uharibifu wa misitu na ukataji miti hovyo
Uharibifu unaoendelea katika maeneo ya kuanzia Msata, Wami hadi Mbwewe kwa kuchoma misitu na mapori hovyo kwa dhana potofu ya kuua wadudu wanaoshambulia mifugo ili kupata nyasi mpya kwa ajili ya malisho na kutayarisha mashamba kunatokana na kukosa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa misitu.
Kutokana na hali hii ipo haja kwa viongozi kuhakikisha wanaelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi misitu na kuacha kubweteka bila kuwachukulia hatua waharibifu hao.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi. Mwantumu Mahiza aliwawajibisha madiwani wa Kata ya Mbwewe na Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo kwa kuwapa siku tatu kuhakikisha kuwa wawe wamewapata watu wanaochoma misitu na mapori kwa makusudi na kwamba endapo watashindwa watawajibika.
Kitendo cha kuwawajibisha viongozi hao kitawakumbusha kuwa makini na kazi zao na kuacha tabia ya kubweteka maofisini pasipo kuwajibika na kiwe mfano kwa maeneo mengine.
Pia Wizara ya Maliasili na Utalii ilikiri kuwa hali ngumu ya uchumi inayoikabili jamii inachangia misitu ya Kanda ya Afrika kupotea kwa kuvunwa hovyo.
Kaimu Mkurugenzi Misitu na Nyuki Bi. Gladness Mkamba hivi karibuni alifungua mkutano wa wadau wa nyuki kutoka nchi za Ukanda wa Mashariki na Kusini juu ya uanzishwaji wa mtandao wa mawasiliano na kukiri kuwa kuwa hali ya misitu ni mbaya kutokana na kuvunwa.
Kutokana na hali hiyo uanzishwaji wa Mtandao wa Mawasiliano kupitia nchi hizo utalenga kutafuta ni namna gani wataweza kuwasiliana ili kuhakikisha wanakabiliana na changamoto zinazoikabili misitu.
Kupitia mtandao huo kutawekwa mikakati ya pamoja kuhakikisha uharibifu wa misitu unatoweka kupitia uwakala ambao watafanya kazi kwa kanda.
Hadi sasa tayari kuna Kanda saba ambazo zitakuwa na maamuzi yake tofauti na awali ambapo maamuzi yalikuwa yakitolewa na Wizara.
Uzoefu unaonyesha kuwa ili kufanikiwa na utunzaji wa misitu ni lazima wananchi wanaoishi maeneo ya kandokando ya misitu wanashirikishwa kikamilifu katika kuilinda.
Kutokana na uchache wa wataalamu si busara kuwatumia wataalamu peke yao kulinda misitu bila kuwashirikisha wananchi.
Kufanya kazi kwa pamoja kwa kutumia mtandao huu kutasaidia kuleta maendeleo kwa sekta ya misitu na nyuki kwani nchi zitashiriki kikamilifu kubadilishana uzoefu.
Kufanya hivyo naamini kutawezesha misitu yetu kuwa katika hali ya usalama na kuangalia njia mbadala ya kuwawezesha wananchi kuangalia ni namna gani wataweza kujikomboa na umaskini.
Ni ukweli kuwa maliasili kwa upande wa misitu imekuwa ikiharibiwa na wananchi kutokana na kuvunwa ili kuweza kupata kuni kwa ajili ya matumizi ya kila siku.
Ili kuondokana na uharibifu wa misitu ipo haja kwa serikali kuwashirikisha wadau wote wakiwemo wananachi kwa kuwapa mbinu mbalimbali za kuwawezesha kujikimu ili kuzuia uharibifu.
Ukweli ni kwamba hali ya misitu kuharibiwa inatokana na hali ngumu ya uchumi inayowakabili wananachi hasa wa kipato cha chini ambao hutumia nishati ya kuni katika kuandaa vyakula.
Tatizo ni ukosefu wa elimu juu ya utunzaji misitu iliyozungukwa na wananchi kwani wengi wao huamini kuwa ni mali ya kijiji.
Ili kufanikiwa na utunzaji wa misitu ni lazima wananchi wanaoishi maeneo ya kandokando ya misitu kushirikishwa kikamilifu katika kuilinda misitu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment