06 September 2012
DC Nkambaku na mikakati ya kuibadili Kishapu
Na Suleiman Abeid
MOJA ya mambo yaliyobeba sehemu kubwa ya mjadala katika bunge la mwezi Aprili mwaka huu, ni taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali nchini (CAG) baada ya kubainika kuwepo kwa wizi katika idara na mashirika mbalimbali ya umma nchini.
Hata hivyo katika tuhuma hizo ubadhirifu mkubwa ulitajwa kufanyika katika halmashauri, Miji na wilaya ambako mamilioni ya shilingi za walipa kodi yalibainika kutafunwa nje ya utaratibu na kuzababisha hasara kubwa katika halmashauri hizo.
Moja ya Halmashauri iliyotajwa kwa kinara cha wizi huo ni halmashauri ya wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga ambako ilielezwa kiasi cha shilingi bilioni 6.7 zilitafunwa na watumishi katika halmashauri hiyo.
Kwa ujumla taarifa hiyo ya CAG kwa mara ya kwanza ilipokelewa kwa shangwe na watanzania wengi ambapo mbali ya kupongezwa ilimlazimu Rais Jakaya Kikwete kubadili safu ya mawaziri wake ambao wengi wao walituhumiwa kuzembea na kusababisha kuwepo kwa upotevu huo wa fedha za umma katika wizara walizokuwa wakiziongoza.
Mbali ya kupoteza kazi kwa baadhi ya mawaziri lakini pia baadhi ya watendaji katika halmashauri kadhaa zilizoguswa na tuhuma hizo hivi sasa wameshafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili huku wengine wakiendelea kuchunguzwa wakiwa wamesimamishwa kazi.
Kutokana na kusimamishwa kwa baadhi ya watumishi katika halmashauri ya Kishapu huku wengine wanne akiwemo mtumishi mmoja wa benki wakipandishwa kizimbani wakituhumiwa kuhusika na wizi huo, sehemu kubwa ya idara za halmashauri hiyo zinaongozwa na watendaji wapya.
Aidha katika mabadiliko hayo, wilaya ya Kishapu pia iliguswa baada ya aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Abdalah Lutavi kuhamishiwa wilaya nyingine na badala yake kupelekwa mpya Bw. Wilson Nkhambaku maarufu kwa jina la “Ngh’ondiyape.”
Akizungumza na wakazi wa mji wa Mhunze katika mkutano wake wa kwanza wa hadhara, Bw. Nkhambaku anasema pamoja na hali tete iliyojitokeza atahakikisha anabadili hali hiyo na kuifanya Kishapu kuwa mpya yenye maendeleo.
Bw. Nkhambaku anasema iwapo viongozi na watendaji wote wilayani Kishapu kwa kushirikiana na wakazi wa wilaya hiyo watashikamana wana uwezo mkubwa wa kubadili hali ya sasa na kuiwezesha wilaya hiyo kuwa mojawapo ya wilaya za mfano katika suala zima la maendeleo kwa wakazi wake.
Anasema baada ya taarifa ya CAG watu wengi waliamini kwamba wilaya hiyo haitoweza kusimama na kuwa imara tena hali ambayo anapingana nayo.
“Si kweli kwamba baada ya kubainika kwa wizi wa kiasi cha shilingi bilioni 6.7 katika halmashauri yetu ya wilaya, basi sasa tukate tamaa na kubweteka katika kufanya kazi za maendeleo, hapana, mimi hilo nalipinga kwa nguvu zote,”
“Naamini kwamba kubainika kwa ubadhirifu huo ni sehemu ya changamoto kwa viongozi na watendaji waliopo hivi sasa madarakani kuona jinsi gani wanaunganisha nguvu zao na kufanya kazi kama kitu kimoja ili kuzuia hali hiyo isitokee tena,”
Anasema baada ya kuwasili wilayani Kishapu amekaa na makundi mbalimbali kuanzia viongozi wa serikali, halmashauri ya wilaya, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wananchi kwa ujumla ambako kote amewaomba kusahau yaliyopita na washikamane katika kufanya kazi za maendeleo.
“Naamini iwapo tutashikamana tutaibadili sura ya wilaya yetu, na hata wale waliokuwa wakiicheka watashangaa, binafsi siku nilipoapishwa kuwa mkuu wa wilaya hii, nilimuahidi waziri mkuu, Bw. Mizengo Pinda kwamba pamoja na watu kunishangaa kwamba napelekwa wilaya yenye matatizo, lakini naamini baada ya muda mfupi nitabadili sura ya Kishapu,”
“Haya yote yatafanikiwa tu kwa viongozi na watendaji wote kushikamana na kuwa kitu kimoja, na kuhakikisha tunawaondolea wakazi wa wilaya yetu kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo udhibiti wa hali ya juu wa ubadhirifu wa fedha za walipa kodi,” anasema Bw. Nkhambaku.
Anasema katika kipindi kifupi alichokaa Kishapu, amebaini uwepo wa kero mbalimbali zinazowakabili, wananchi ambazo ameahidi kuzipatia utatuzi wa haraka kwa kadri itakavyowezekana huku akiitaja moja ya kero kubwa inayopigiwa kelele ni migogoro ya ardhi inayosababishwa watumishi wa idara ya ardhi.
“Nimepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakiwalalamikia watumishi wa idara hii ya ardhi, nimewapa maelekezo na kuwataka wabadilike haraka, vinginevyo nitahakikisha nakufa nao, na ikishindikana basi aidha niondoke mimi au wao,”
“Kwa kweli ukiwasikiliza wananchi, utawahurumia, yapo mambo wala hayahitaji mwananchi azungushwe, lakini yalikuwa yakifanyika, inakuwaje mwananchi anayehitaji kupatiwa hati ya kumiliki ardhi aliyopewa aombwe kwanza atoe nauli ya kufuatilia hati hiyo wizarani,? Huu si utaratibu,” anasema Bw. Nkhambaku.
Pia anasema tatizo lingine la wilaya yake ni kuporomoka kwa kiwango cha elimu miongoni mwa watoto mashuleni ambapo matokeo ya mitihani ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na wale wa kidato cha nne si mazuri na kuifanya wilaya hiyo mara nyingi kuwa ya mwisho kimkoa katika mitihani hiyo.
Anasema yapo mambo yanayochangia kushuka kwa taaluma ya elimu katika wilaya hiyo lakini kwa sehemu kubwa wakazi wake bado wana uwezo wa kukabiliana nayo na kuyamaliza na kuwezesha kuinua kiwango cha taaluma.
Anafafanua kwamba baadhi ya mambo yanayochangia kushuka kwa kiwango cha elimu katika wilaya hiyo ni baadhi ya walimu kutotimiza wajibu wao kikamilifu na wengine wakijihusisha na vitendo vya kufanya biashara huku wakisahau wajibu wa kufundisha watoto.
Anasema, “Pamoja na uhaba wa walimu lipo tatizo la vitendea kazi, ikiwemo uhaba wa vitabu vya kujifunzia na kufundishia, madawati na nyumba za kuishi walimu, tumeweka mkakati wa kuhakikisha tunashughulikia haraka matatizo hayo ikiwemo suala la madawati,”
“Tunataka ifikapo Desemba 31, 2012 tuhakikishe tumemaliza tatizo la madawati, kwa ushirikiano wa jamii naamini kero hii tutaitatua, lakini pia tumewaagiza watu wa idara ya elimu ukaguzi watimize wajibu wao, wawadhibiti walimu wote watoro kazini, kwa kuhakikisha wanafundisha kikamilifu idadi ya vipindi wanavyopaswa kufundisha.”
Anasema kuanzia sasa hatosita kumchukulia hatua za kinidhamu mwalimu atakayebainika kwenda kinyume na maadili yake ya kazi ikiwemo wanaovaa mavazi yasiyo na heshima mbele ya wanafunzi wao.
Kwa upande wa watumishi wa halmashauri ya wilaya ambao wamezoea kufanya kazi zao kwa mazoea, mkuu huyo anasema ni bora sasa wakubali kubadilika maana hatokuwa na aibu ya kumwajibisha mtumishi atakayebaini kuzembea au kwenda kinyume na maadili yake ya kazi.
“Nimetangaza vipaumbele vyangu vya kwanza kabisa ambavyo nitahakikisha nakufa navyo mpaka vifanikiwe, ambavyo ni pamoja na suala la elimu, afya, kilimo sambamba na suala zima la ulinzi na usalama kwa wananchi wetu,” anaeleza Bw. Nkhambaku.
Anasema kwa upande wa kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa watanzania, atahakikisha anawahamasisha wakulima wakubali kuachana na kilimo cha kizamani walichorithi kutoka kwa mababu na waweze kulima kilimo chenye tija na kitakachowawezesha kuondokana na umaskini.
“Mimi naamini hakuna lisilowezekana iwapo tutaamua, hivyo nimewahimiza wakazi wa Kishapu kwa kushirikiana na wawakilishi wao madiwani tushikamane kwa dhati katika kazi za maendeleo na tuweze kuibadili wilaya yetu iwe ya mfano nchini kwa uzalishaji mali,”
“Lakini pamoja na haya yote nimewaomba ndugu zangu wa Jeshi la Polisi wabadilike, maana iwapo wilaya haitokuwa na utulivu ni wazi hakuna jambo lolote la maana la kimaendeleo linaloweza kufanyika, yapo malalamiko dhidi ya polisi ambayo nimeyapokea, lakini nimewaelekeza viongozi wao nini cha kufanya,” anasema Bw. Nkhambaku.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment