06 September 2012
Champion kuanza mazoezi mapema
Na Andrew Ignas
UONGOZI wa timu ya Champion Academy ya Tanganyika Packers Kawe, Dar es Salaam umewataka wachezaji wake kuanza mazoezi Septemba 18, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa timu hiyo, Willium Mamuro alisema kikosi chake kinatakiwa kuanza mapema ili kujiandaa na michuano ya Sparaestare.
Alisema mashindano hayo yanatarajia kufanyika Desemba mwaka huu, baada ya awali kuahirishwa kutokana na kuupisha mwezi wa Ramadhan.
"Tunatarajia mazoezi yataanza mwezi huu tarehe 18, hivyo tunawahimiza wachezaji wetu kufika kwa wakati ili kujiandaa vyema na mashindano hayo," alisema.
Alisema hivi sasa wapo katika mchakato wa kukiimarisha kikosi chake, baada ya kuona kuna upungufu katika safu ya ushambuliaji, beki na kiungo.
"Katika kikosi changu cha vijana wenye umri chini ya miaka 16 tuna upungufu mkubwa katika nafasi hizo nilizokwambia, ndiyo maana tumepania kuanza mazoezi mapema ili kuufanyia kazi upungufu huo," alisema.
Alisema katika mashindano ya mwaka huu ambayo yamedhaminiwa na hoteli ya Mediteranio zawadi kwa bingwa zitakuwa jezi seti moja, kombe, medali za dhahabu na sh. 10,000 kwa kila mchezaji kwa mshindi wa kwanza.
Mwenyekiti huyo alisema mshindi wa pili atajinyakulia medali za shaba na sh. 5000 kwa kila mchezaji, wakati wa tatu atapata medali za fedha kwa kila mchezaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment